Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Serikali Yaagiza Usalama Migodini Lindi


Serikali ya Awamu ya Sita imesema itahakikisha usalama na afya ya Watanzania wanaofanya kazi kwenye migodi ya dhahabu na graphite mkoani Lindi inazingatiwa kikamilifu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu alipotembelea migodi ya Lindi Graphite Technologies Ltd na mgodi wa dhahabu wa Elianje Genesis Ltd (Namungo) wilaya ya Ruangwa 04 Agosti 2026 kukagua uzingatiwaji wa sheria za usalama mahala pa kazi.

Waziri Sangu alisema kipaumbele cha serikali ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanafanya kazi katika mazingira salama na yenye staha, ili wachangie ipasavyo katika uchumi wa taifa huku afya zao zikilindwa.

Alitoa rai hiyo baada ya kukagua maendeleo ya migodi hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.

Waziri huyo ameagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kuendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa migodi na wachimbaji kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za usalama katika maeneo hayo muhimu kiuchumi.

"Naipongeza OSHA kupitia Mtendaji Mkuu wake kwa kuendelea kusimamia usalama na afya mahala pa kazi. Lengo ni kuhakikisha fedha mnazopata kwenye migodi hii zinawafaidi mkiwa na afya njema," alisisitiza Sangu.

Waziri Sangu alisema pia dhamira ya serikali ni kuhamasisha sekta binafsi kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050, ili sekta hiyo ichangie asilimia 70 ya pato la taifa kama ilivyokusudiwa ikiwemo kuzalisha ajira kwa watamzania wengi.

Kwa upande wake, kijana Benard Denis akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Lindi Graphite Technologies, alieleza changamoto ya kutotolewa vifaa vya kujikinga pamoja na kupewa kazi tofauti na zilizopo kwenye mikataba.

"Tulisaini mikataba ya waendesha mitambo lakini wakati mwingine tunapewa kazi ya matope kwenye mgodi. Hii inaathiri usalama wetu na tunaomba serikali iingilie kati," alisema Denis.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Sangu aliagiza uongozi wa mgodi huo kuweka mazingira salama kwa wafanyakazi, na kuitaka OSHA kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kuwa kiwanda hicho kimeanza uzalishaji rasmi mwezi mmoja uliopita.

Katika taarifa yake, Afisa Utumishi wa Lindi Graphite, Clement Mvuma alisema mgodi huo umetoa ajira 230 kwa Watanzania na 15 kwa wageni. Pia umeanza kuzalisha tani 2,000 za graphite, kwa wastani wa tani 70 hadi 80 kwa siku.

Naye Katibu wa Wachimbaji wa mgodi wa dhahabu wa Elianje Genesis Ltd alisema mgodi huo umetoa ajira za moja kwa moja 4,678 na zisizo rasmi 3,250, jumla ya ajira 7,928 zimepatikana kwa watanzania.

Kwa upande wake, John Mashauri Mfanyakazi Mgodi wa Dhahabu wa Elianje Genesis Ltd (Namungo) ameishukuru Serikali kupitia OSHA kwa kuwapatia mafunzo kuhusu masuala ya Usalama na Afya.

Waziri Sangu anaendelea na ziara yake Lindi na leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Siku ya Korosho kwenye Maonesho ya Nane Nane pamoja na kuzungumza na Baraza la Wazee Wilaya ya Lindi.