Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

GGM yapongezwa uzingatiaji sheria fidia kwa wafanyakazi


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imesema mazingira wezeshi ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita yamewezesha Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kutekeleza kikamilifu sheria za kazi na kulinda ustawi wa wafanyakazi na jamii inayouzunguka mgodi.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu, wakati kamati ilipotembelea kukagua utekelezaji wa Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika mgodi huo uliopo Manispaa ya Geita, Septemba 22, 2026.

Mhe. Mchafu amesema GGM umetekeleza kikamilifu sheria ya WCF, ambapo michango na fidia kwa wafanyakazi zinalipwa kwa wakati, hatua inayoonesha dhamira ya kampuni katika kuleta ustawi wa jamii.

Aidha, Mwenyekiti huyo ameitaka Menejimenti ya mgodi kuongeza ushirikishwaji wa jamii inayouzunguka mgodi ili miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) iwanufaishe wengi zaidi.

Mgodi huo umesisitizwa kuzingatia udhibiti endelevu wa vihatarishi kazini ili kulinda afya za wafanyakazi wakiwa kazini na hata baada ya kustaafu.

Vilevile, Mhe. Mchafu ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuuwezesha mgodi wa Geita kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, hatua inayohakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kupunguza gharama za uzalishaji.

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Dkt. Evaline Munisi, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Mhe. Deus Sangu, amesema mgodi umetoa ajira zaidi ya 7,000 ikiwemo za moja kwa moja 2,311 na zisizo za moja kwa moja 4,742 kwa Watanzania.

Kuhusu michango ya WCF, Dkt. Munisi ameeleza kuwa katika mwaka 2025/26, kiasi cha Shilingi milioni 784 kilichangwa na wafanyakazi, huku katika robo ya kwanza ya mwaka 2026/27, mgodi umechangia Shilingi milioni 198. Hadi sasa, WCF imeshalipa kiasi cha Sh. milioni 676 kama fidia kwa wafanyakazi.

Dkt. Munisi ameongeza kuwa WCF imepokea jumla ya madai 61, na kati yake madai 54 sawa na asilimia 87 yameshashughulikiwa, hatua iliyoleta faraja kwa wafanyakazi waliofikwa na majanga kazini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendelezaji na Mahusiano wa GGM, Gilbert Mworia, amesema kipaumbele cha kampuni ni kuhakikisha haki na afya za wafanyakazi zinalindwa muda wote, na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote ya Kamati ya Bunge