News
Kamati ya Bunge Yaitaka OSHA kufanya ufuatiliaji wa masuala ya Usalama na Afya za Wafanyakazi katika maeneo ya Kazi
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeitaka Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) kuwa na utaratibu maalum wa kufuatilia usalama na afya za wafanyakazi katika maeneo ya kazi ili wanaobainika kuwa na changamoto za kiafya baada ya kufanyiwa uchunguzi waweze kupata huduma na msaada unaostahili.
Maagizo hayo yametolewa leo Agosti 12, 2026 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Chakoma Mchafu, wakati kamati hiyo ikipokea taarifa ya utekelezaji wa Taasisi ya OSHA katika kipindi cha Mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza mara baada ya kupokea na kujadili taarifa ya OSHA, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu, amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024, OSHA ilifanya uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi 845, ambapo wafanyakazi 274 walibainika kuwa na magonjwa mbalimbali.
Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuwa na utaratibu wa kudumu wa kuwafuatilia wafanyakazi wanaokuwa na changamoto baada ya uchunguzi na kuchukua hatua haraka, badala ya kuishia katika hatua ya kubaini changamoto za afya pekee.
“Kamati inashauri kuwe na mfumo au utaratibu wa kufanya ufuatiliaji kwa wale wafanyakazi ambao watakuwa wamebainika kuwa na matatizo ya afya, ili waweze kufuatiliwa na kusaidiwa kutatuliwa changamoto zao,” amesema.
Kadhalika, Mhe. Mchafu ameitaka OSHA kuendelea kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, ameongeza kuwa elimu endelevu ni muhimu kutokana na mabadiliko ya teknolojia.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amesema kuwa suala la usalama na afya mahali pa kazi ni jambo la msingi katika kujenga mazingira bora na yenye tija kwa wafanyakazi.
“Ili tuweze kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 tunahitaji nguvu kazi salama na yenye afya, hivyo tunakupongeza Mwenyekiti na Kamati yako kwa kusimamia kwa karibu suala hili na kuendelea kutoa maelekezo ambayo yamekuwa na tija" amesema
Awali, akizungumza wakati akiwasilisha taarifa, Naibu Waziri, fisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Dkt. Evaline Munisi amesema utekelezaji wa Sheria na Kanuni za usalama na afya mahali pa kazi umeendelea kuleta matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa mwitikio wa waajiri kusajili maeneo ya kazi OSHA.
Naye, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa wataendelea kutoa elimu kwa wadau ili kuhakikisha maeneo yote ya kazi yanakuwa salama, yenye afya na yanayochangia maendeleo endelevu ya uchumi wa Taifa.



