Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Kamati ya Bunge Yaridhishwa na Uimarishaji Mfuko wa PSSSF


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, imeridhishwa na dhamira ya serikali ya kuimarisha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ikiwamo kulipa Sh.Trilioni 2.17 ambazo ni sehemu ya deni la michango ya watumishi wa kabla ya Mwaka 1999.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe.Fatuma Toufiq ameyasema hayo Oktoba 19, 2023 katika kikao cha kamati hiyo cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya PSSSF uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Amesema kamati inampongeza Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mfuko huo ambapo Desemba 15, 2021 serikali ilitoa fedha hizo na kulipa madeni ya uwekezaji sh.Bilioni 500 kati ya Sh.bilioni 731 zilizohakikiwa.

Mhe. Toufiq amehimiza mfuko kutoa elimu ya kujiandaa kustaafu kuanzia kwa waajiriwa wapya ili wafanye maendeleo na kujiwekea akiba mapema badala ya kusubiri hadi wastaafu.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Prof.Joyce Ndalichako, amesema serikali itaendelea kuimarisha uhai wa mfuko huo na kuahidi kufanyia kazi ushauri uliotolewa na kamati hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe.Patrobas Katambi, amesema serikali imetengeneza mifumo ya kisheria inayolenga kuleta ustawi kwa watumishi wanapostaafu.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, amesema hatua zingine zilizochukuliwa na serikali kuboresha mfuko huo ni pamoja na kuzuia uwekezaji kwenye maeneo yasiyo na tija na kuweka ukomo wa uwekezaji ili kuleta ufanisi.