Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu: Watanzania Tulinde Umoja wa Taifa letu


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amewahimiza Watanzania kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na amani kwa kuwa ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Waziri Sangu ametoa wito huo leo Julai 19, 2026 aliposhiriki Ibada ya Jumapili katika kanisa la Parokia ya Msalaba Mtakatifu – Muze wilaya ya Sumbawanga Mkoa wa Rukwa, ambapo amewataka wananchi kuendelea kuwa wamoja, kushirikiana na kuenzi tunu za Taifa zinazochangia kudumisha amani.

"Nchi yetu imebarikiwa kuwa na amani na umoja, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda na kurithisha kwa vizazi vijavyo ili kuishi kwa upendo bila kujali tofauti zetu," amesema Waziri Sangu.

Sangu aliongeza kusema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuendeleza mahusiano mema ndani ya jamii ili Watanzania waendelee kufaidi amani iliyopo kwani ndilo taifa tulilopewa na Mungu.

Kwa upande wake, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Msalaba Mtakatifu – Muze, Padri Peter Twamba, ameishukuru Serikali kwa kuanzisha Wizara inayosimamia masuala ya Mahusiano, na kueleza kuwa hatua hiyo imeisaidia kuimarisha uratibu wa makundi mbalimbali ya kijamii yanayogusa ustawi wa wananchi.

"Taasisi za dini kwa kushirikiana na Serikali zina jukumu kubwa la kujenga na kuimarisha ustawi wa binadamu pamoja na kudumisha maadili na mshikamano wa jamii," amesema

Kadhalika, amempongeza Waziri Sangu kwa kazi anazofanya ndani ya Wizara anayoisimamia inavyoratibu masuala ya mahusiano kati ya makundi mbalimbali ya jamii bila kujali tofauti zao.