Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Kamati ya Bunge Yaridhishwa na uzalishaji wa kiwanda cha sukari Mkulazi


Serikali imeendelea kutekeleza mikakati iliyoanishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia uwekezaji wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kinachomilikiwa kwa ushirikiano kati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza.

Uwekezaji huo umetajwa kuwa miongoni mwa miradi ya kimkakati inayochangia kukuza uchumi wa nchi, kuongeza uzalishaji wa ndani wa sukari pamoja na kufungua fursa nyingi za ajira kwa Watanzania.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, wakati wa ziara ya ukaguzi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi iliyofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Hawa Mchafu, leo Mei 23, 2026 mkoani Morogoro.

Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Sangu ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kuendelea kufuatilia na kusimamia maendeleo ya mradi huo, akibainisha kuwa maelekezo yote 11 yaliyotolewa na kamati katika ziara zilizopita tayari yameingizwa katika mpango wa utekelezaji.

Amesema hatua hiyo inaonesha namna Bunge linavyotekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali kwa kutoa ushauri, maelekezo na kuhakikisha sheria na kanuni zinafuatwa kwa maslahi ya wananchi.

Aidha, Waziri Sangu amesema Serikali ina matarajio makubwa kupitia uwekezaji huo ambapo takribani ajira 11,000 zinatarajiwa kuzalishwa kwa vijana katika nyanja mbalimbali za uzalishaji na huduma. Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha mifuko ya hifadhi ya jamii inawekeza katika miradi yenye tija kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.

Sambamba na hilo, Waziri Sangu amesema kiwanda hicho kinaendelea kutekeleza mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia mwaka 2024/2025 hadi 2028/2029, ambapo uzalishaji wa miwa utaongezeka kutoka hekta 3,600 hadi hekta 4,156. Aidha, uzalishaji wa sukari unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 20,000 hadi kufikia tani 50,000 ifikapo Juni 30, 2028.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Evaline Munisi, ameipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa kujitoa kwake katika kuhakikisha jamii inayozunguka kiwanda inanufaika na uwekezaji huo kupitia ajira, miradi ya kijamii na maendeleo ya kiuchumi. Amesema kamati hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.

Dkt. Munisi pia amepongeza uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi kwa kufikia asilimia 96.4 ya malengo waliyojiwekea katika uzalishaji wa sukari, hatua ambayo imeonesha mafanikio makubwa tangu kuanza kwa uzalishaji rasmi wa kiwanda hicho. Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji kuhakikisha kiwanda kinaongeza ufanisi na kuendelea kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Kafiti William Kafiti, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Hawa Mchafu, amesema kiwanda hicho kimekuwa kikikua mwaka hadi mwaka na kinatarajiwa kuzalisha zaidi ya tani 38,000 za sukari ifikapo mwaka 2026/2027.

Mhe. Kafiti ameeleza kuwa uwekezaji huo umekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima wa miwa, wananchi wa maeneo jirani pamoja na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutokana na faida zinazotokana na uwekezaji huo.

Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi, Mhandisi Flavian Reginald, amesema kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda vichache nchini vinavyozalisha sukari za aina mbili ambazo ni sukari ya majumbani (brown sugar) na sukari nyeupe kwa matumizi ya viwandani.

Amesema kiwanda kinaendelea kuboresha mifumo ya umwagiliaji katika mashamba yake ili kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za uendeshaji na kuhakikisha kiwanda kinapata faida endelevu kila mwaka.