News
Kamishina Mkangwa: Fanyeni kaguzi zenye Tija
Serikali imetoa wito kwa Maafisa Kazi nchini kuimarisha usimamizi wa sheria ya kazi Nchini, kufanya kaguzi zenye tija na kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi, hatua inayolenga kujenga mahusiano bora na kuongeza ufanisi katika maeneo ya kazi.
Wito huo umetolewa leo Septemba 04, 2026 Jijini Dodoma na Kamishna wa Kazi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Suzan Mkangwa, wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Kazi kwa mwaka 2025/26 kwa Maafisa Kazi Wafawidhi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, ambapo amesema hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha sheria za kazi zinatekelezwa ipasavyo na majukumu mengineyo.
Amesema kuwa kikao hicho kina lengo la kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyofanyika katika mwaka wa fedha uliopita na kupitia mpango kazi wa mwaka 2026?27 na kujengeana uwezo katika masuala ya utekelezaji wa Sheria za kazi, utawala na taarifa za soko la ajira pamoja na masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi.
Ameongeza kuwa kikao hicho kinatoa nafasi kwa watumishi kutafakari mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na kuweka mikakati madhuburti ya kuboresha utekelezaji wa majukumu ya idara katika mwaka mpya wa fedha.
Aidha amewapongeza kwa mafanikio waliyoyapata kwa mwaka wa fedha uliopita kwa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kusimamia utekelezaji wa amri ya kima cha chini cha mshahara, ushirikishwaji wa wafanyakazi kupitia mabaraza ya wafanyakazi na kuratibu mashauriano kati ya Serikali, waajiri na vyama vya wafanyakazi pia kusimamia na kuratibu ajira za wageni.
Hata hivyo, Kamishna Mkangwa amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo, amewahasa wafawidhi hao kuendelea kuimarisha usimamizi wa sheria katika maeneo ya kazi, huku akiwataka watumishi kufanya kaguzi zinazolenga kuleta matokeo chanya.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia ni jambo lingine linalopaswa kupewa kipaumbele, huku akiwataka watumishi kuanza kutumia kikamilifu Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Soko la Ajira, ambao utasaidia kuboresha upatikanaji na usimamizi wa taarifa za soko la ajira nchini.
Akizungumza awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dkt. John Mduma amesema kuwa WCF inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano kupitia Idara ya Kazi, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu haki, wajibu na taratibu za kupata fidia pindi wanapopata ajali, kuugua au kufariki kutokana na kazi.
Amesema kuwa Ushirikiano huo unalenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu na kuongeza uelewa kuhusu mfumo wa fidia na kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wadau wa soko la ajira katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Mikoa na Wilaya ambazo WCF haijawa na ofisi za moja kwa moja.



