Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Serikali, Wadau wazungumzia changamoto za sekta ya Usafirishaji


Serikali na wadau wa sekta ya usafirishaji wajadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo upatikanaji wa mafunzo na elimu kwa madereva pamoja na hatua za kuimarisha usalama barabarani.

Majadiliano hayo yamefanyika Septemba 29, 2026, katika kikao cha kutathmini utekelezaji wa hoja za vyama vya wafanyakazi, madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, kilichofanyika katika Ofisi za OSHA jijini Dodoma.

Akizungumza Mwenyekiti wa kikao hicho, Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Susan Mkangwa, amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wadau kuhusu umuhimu wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi, hususan wamiliki na viongozi wa sekta ya usafirishaji.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO), SSP Yussuf Kamotta, amewataka wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kuwawezesha madereva kupata elimu na mafunzo yatakayowaandaa kupata leseni za udereva, hasa wale wanaohitaji msaada zaidi katika masuala ya elimu.

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Malori Tanzania (TAMSTOA), Chuki Shabani, amesema kuna haja ya kuwepo kwa mfumo bora wa utoaji elimu kwa madereva kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), hususan kwa wanafunzi wanaomaliza mafunzo ya udereva kabla ya kuanza kutumia barabara.

Amesema mfumo huo utasaidia kuhakikisha madereva wanaoingia katika sekta hiyo wanakuwa na uelewa na maandalizi yanayohitajika, hatua itakayochangia kuimarisha usalama barabarani na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji.