News
Mhe. Ridhiwani Kikwete abainisha mikakati ya kukuza Ajira
SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeanza mchakato wa kurejea sera ya ajira ambayo imesheeni mikakati ya kukuza ajira nchini.
Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameyasema hayo leo Novemba 15, 2024 alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa nane wa kazi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) jijini Dodoma.
Amesema mkazo mkubwa umewekwa kwenye mazingira wezeshi kwa ajili ya vijana kujiajiri na kuwajengea uwezo wa kuajirika.
“Hapa tunazungumzia sera ya kazi ya kujitolea, sera za ajira za muda mfupi na mrefu, na sera inayotambua uwepo wa wenzetu waliosomeshwa vizuri lakini bado wanazurura hawana kazi,”amesema.
Pamoja na hayo, amekemea baadhi ya vyama ambavyo vimekuwa na migogoro ya uongozi na kwamba serikali inahitaji vyama imara vinavyoweza kushiriki kikamilifu na kwa weledi kwenye meza ya majadiliano.