Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu aitaka CWT kulinda maslahi ya Wanachama


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amekitaka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuwa nguzo muhimu katika kulinda na kutetea maslahi ya wanachama ikiwemo kutatua kero zinazowakabili wanachama katika maeneo yao ya kazi.

Amebainisha hayo wakati akifungua kikao cha Baraza la Taifa la Chama cha Walimu Tanzania leo Februari 07, 2026 Jijini Dodoma, ambapo ametoa msisitizo kwa chama hicho kusimamia nidhamu, weledi na uzalendo ili kuhakikisha haki na wajibikaji wa wanachama wake.

Aidha, Waziri Sangu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza Mikataba ya Kimataifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ikiwemo mashauriano ya Utatu yaani Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri.

Kadhalika, Mhe. Sangu amesema Serikali imeendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kutoa ajira mpya kwa walimu na kuimarisha maslahi ya walimu.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Selemani Ikomba amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha maslahi ya Walimu nchini yanaendelea kulindwa.