Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

NAIBU WAZIRI IKUPA AWAOMBA WADAU KUJITOKEZA MAPAMBANO DHIDI YA MADAWA YA KULEVYA


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera anayeshughulika Wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa ameelezea jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kupambana na dawa za kulevya nchini.

Akizungumza Naibu Waziri Ikupa alisema kuwa tatizo la dawa za kulevya limekuwa likileta athari kubwa katika jamii hivyo jitihada za wadau katika vita hiyo ni muhimu sana katika mapambano ya madawa ya kulevya.

“Tunawapongeza Binti Filamu kwa kuandaa tamasha hilo linalofahamika kwa jina la Kataa mihadarati. Athari za dawa za kulevya kwa namna moja au nyingine zinamgusa kila mtu kwenye jamii yetu. Serikali katika kuhakikisha inakomesha dawa za kulevya iliamua kuunda mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo hakika imefanya kazi kubwa,” amefafanua Ikupa.

Ametoa ushauri kwa Binti Filamu kuhakikisha katika matamasha yanayokuja waende kwenye mikoa ambayo athari za matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na kwa kufanya hivyo watasaidia kuikoa jamii kupitia elimu ambayo wanaitoa kuhusu madhara yatokanayo na utumiaji wa dawa hizo. Kuhusu mapendekezo ambayo yametolewa na wadau mbalimbali kwenye tamasha hilo yakiwemo ya Serikali kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu dawa za kulevya amesema ameyachukua na watayafanyia kazi kwani ni mambo yanayowezekana.

Kwa upande wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) limeshauri kwamba ufike wakati sasa kuwepo na sera ambayo itahimiza mashirika, taasisi na wadau mbalimbali kushiriki kwa vitendo katika mapambano dhidi ya vita ya dawa za kulevya nchini. Ushauri huo umetolewa leo Desemba 28,2018 na Ofisa Masoko wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) Israel Severe wakati wa tamasha la Kataa Mihadarati liloandaliwa na Taasisi ya Binti Filamu chini ya Mwenyekiti wake muigzaji maarufu wa filamu Ndumbagwe Misayo anayetambulika kwa jina la Thea.

“Shirika la Bima la Taifa Tanzania tumeamua kushiriki kwenye tamasha hilo kutokana na kutambua umuhimu wake kwa jamii.Tunajua moja ya jukumu letu ni kushughulika na mambo ya bima lakini kwetu ni muhimu zaidi kuona jamii tunayoihudumia inakuwa salama kiafya.Sote tunatambua athari za matumizi ya dawa za kulevya, hivyo tumeamua kushiriki kikamilifu kwenye vita hii ili kukomesha dawa hizo nchini.

Tunashauri ifike wakati kuwe na sera ambayo itazungumzia umuhimu wa mashirika na taasisi mbalimbali nazo kushiriki kwenye vita hii ya dawa za kulevya. Hivyo ni wakati muafaka kwa Serikali kuweka sera itakayokwa chachu kwa mashirika na taasisi zote kushiriki kwa vitendo na iwe ni wajibu wetu.

Kuhusu tamasha hilo, Severe amesema anaupongeza uongozi wa Binti Filamu kwa uamuzi wake wa kuandaa tamasha hilo lenye lengo la kutoa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wao ambao wamedhamiria kwa dhati kukomesha dawa hizo nchini kwetu.

“Tunawapongeza Binti Filamu kwa kuandaa tamasha hilo ambalo kwetu sisi tunaona ni mwanzo mpya kwa wasanii kuamua kushirikiana na wadau wengine kukomesha dawa za kulevya.Wanastahili kuendelea kuungwa mkono na sisi NIC tutaendelea kuwaunga mkono kadri watakavyokuwa wanaandaa matamasha haya ya kukataa mihadarati,”amesema Severe.

Wakati huo huo Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Simon Mwakifamba ambaye pia ni Katibu wa Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam amesema umefika wakati wa kuunga mkono juhudi za Rais Dk.John Magufuli katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Amesema kuna wasanii wengi wamekuwa wakijihusisha aidha kutumia dawa za kulevya au kugeuzwa makontena wa kubeba dawa hizo kwa maslahi ya wafanyabiashara lakini madhara yake ni makubwa, hivyo umefika wakati wa kukataa kuwa sehemu ya makontena na watumiaji wa dawa hizo.

Akizungumzia tamasha hilo msanii wa muziki wa Bongo Fleva Haruna Kahena (Inspekta Haroun) amesema kitendo cha Binti Filamu kuandaa tamasha hilo ni wazi wameonesha dhamira njema ya kupambana na dawa za kulevya ambapo kwa sehemu kubwa wapo baadhi ya wasanii wamekuwa wakiyatumia.