Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Naibu Waziri Katambi Awataka Boda Boda Suala la Afya Walipe Kipaumbele


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Patobasi Katambi amewataka Vijana wanaojishughulisha na biashara ya kuendesha pikipiki maarufu kama Boda Boda kuhakikisha wanazingatia Afya zao na masuala ya Usalama Barabarani ili kazi hiyo wanayoifanya iweze kuwa ya tija badala ya kuwaumiza Afya zao.

Mhe. Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini, ameyabainisha hayo wakati alipokuwa akiongea na Vijana wa mjini Shinyanga wanaoendesha piki piki katika Manispaa hiyo, Amewataka kuhakikisha suala la Afya zao kulipa kipaumbele ili waweze kuwa na uhakika wa kujipatia kipato kupitia kazi hiyo.

“Afya ndo msingi wa Uchumi, niwasisitize vijana lazima masuala ya Afya zenu muyajali, ikiwemo kuhakikisha mnazingatia sheria za usalama Barabarani,"

"Serikali itaendelea kutoa elimu juu ya ulinzi na Usalama wenu, ili mpate uwezo wa namna bora ya kutumia barabara katika kufanya kazi hii ya kuendesha pikipiki,” alieleza

Aliongeza kuwa serikali inaendelea na mipango ya kuhakikisha ajira hiyo inakuwa ya tija ikiwemo kuwsajili, kuwaunganisha na Bima za Afya, kupata fursa za mikopo, hivyo wanatakiwa kuwa na umoja na nidhamu kwa jamii na Serikali.

Wakiongea kwa nyakati tofauti, Waendesha Boda Boda, wameshukuru kwa jitihada zinazofanywa na serikali katika kuboresha mazingira yao ya kazi. Aidha, wamemuhakikishia Mhe. Katambi kuwa wataendelea kuzingatia masuala ya Usalama barabarani ikiwemo kuvaa kofia ngumu na makoti maalum, pamoja na kuhakikisha wanaunda vikundi.