Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu ahimiza Jamii kuenzi mshikamano


‎Jamii imetakiwa kuimarisha na kuenzi ushirikiano kupitia majadiliano hatua itakayosaidia kujenga Taifa lenye ustawi kwa maendeleo endelevu.

‎Wito huo umetolewa na Mbunge wa Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi- Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu wakati wa ziara yake katika Kata ya Laela na Kata ya Kasanzama zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa Februari 24, 2026 iliyolenga kuhamasisha ushirikiano, mshikamano na kuimarisha mahusiano ya jamii.

‎Akiwa katika mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa 400Kv wa gridi ya taifa unaotekelezwa kutokea Tunduma hadi Sumbawanga Waziri Sangu aliwaelekeza kampuni ya Sinohydro Corporation Limited kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa umakini ili wananchi wa Sumbawanga wapate umeme wa uhakika .

‎Waziri huyo alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili wananchi wanufaike na kuboresha maisha yao.

‎ Katika hatua nyingine Waziri Sangu alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi pamoja na mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu, huku akipongeza juhudi zinazofanywa na mkandarasi Sino- Hydro katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa viwango vinavyokidhi matakwa ya kisheria na kitaaluma.

‎Aidha Sangu alielekeza mkandarasi huyo kuzingatia hususani suala la Usalama na Afya Mahala pa Kazi pamoja na kuitaka kampuni hiyo kuendelea kuchangia katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kulipa michango ya wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria.

‎Akitoa wasilisho mbele ya Waziri , mwakilishi wa kampuni ya Sino- Hydro ambaye pia ni Meneja Rasimaliwatu na Mahusiano Maghembe Noni aliahidi kuwa kampuni itandelea kushirikiana na Serikali bila kusahau kufuata sheria na taratibu za kazi.

‎Waziri Sangu yupo katika ziara ya kikazi katika Jimbo lake la Kwela ambapo alikagu pia miradi ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana Rukwa iliyopo kata ya Laela na Shule ya Uchile Sekondari iliyopo kata ya Kasanzama.