News
Sangu Atoa Uhakika Usalama Ajira Nje ya Nchi, Awahimiza Vijana Kuzichangamkia
Serikali imewahimiza Watanzania kuchangamkia fursa za Ajira nje ya nchi zinazoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, huku ikiwatoa hofu kuhusu usalama wao wakiwa ughaibuni.
Akizungumza Februari 20, 2026 jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya udereva wa bodaboda na bajaji katika Chuo cha VETA, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amesema Serikali imeandaa mtaala maalum wa kuwaandaa Vijana kabla ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Mhe. Sangu amesema mtaala huo unawajengea vijana uelewa wa sheria, tamaduni na mazingira ya kazi ya nchi wanazokwenda na kuwapa maadili ya kazi, nidhamu na stadi za mawasiliano zitakazowawezesha kuhimili ushindani wa kimataifa.
Amesisitiza kuwa, kazi zinazopatikana nje ya nchi ni zenye staha na zinalindwa kisheria hivyo Serikali itaendelea kuratibu fursa za Ajira ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.
Katika hatua nyingine, amewahamasisha waendesha bodaboda na bajaji kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ukiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupitia mpango wa Hifadhi Scheme kwa sekta isiyo rasmi, ili kujikinga na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amewahimiza wabunge kote nchini kufuata nyayo za Mbunge wa Ilemela Kafiti Kafiti, kwa kuimarisha ushirikiano na VETA ili kuanzisha na kuendeleza mafunzo ya amali yatakayowaongezea vijana ujuzi.
Naye Mbunge wa Ilemela, Mhe. Kafiti ameishukuru Serikali kwa kuendelea kufungua milango ya Ajira nje ya nchi, akisema hatua hiyo inawapa fursa viongozi wa majimbo kuwaandaa vijana wao kunufaika na nafasi hizo.
