Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu azitaka Kampuni kuzingatia sheria za kazi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu ameagiza kampuni zote nchini kuzingatia kikamilifu sheria za kazi na kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa stahiki zao kulingana na viwango vilivyoainishwa katika Sheria za kazi. Aidha, amesisitiza pia utekelezaji wa Amri ya Kima cha Chini cha Mshahara.

Waziri Sangu ametoa agizo hilo Februari 25, 2026, alipotembelea mradi wa ujenzi wa Daraja la Mto Chombe katika Barabara ya Kaoze – Kianda, unaotekelezwa na Kampuni ya Mselem Building and Civil Engineering Co. Ltd, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Rukwa jimbo la Kwela.

Amesema kuwa Serikali tayari imeshatoa maelekezo kuhusu utekelezaji wa amri ya Kima cha Chini cha Mshahara, na kusisitiza kuwa kila mwajiri anapaswa kuhakikisha mfanyakazi analipwa kwa kuzingatia viwango vilivyotangazwa na Serikali.

Akizungumzia suala la Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Waziri Sangu amemwagiza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anazingatia Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ili kulinda nguvu kazi ya Taifa na kuzuia ajali pamoja na madhara yanayoweza kuepukika.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amemsisitiza mkandarasi huyo kuhakikisha anawasilisha michango ya wafanyakazi wake kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), pamoja na michango ya WCF kwa wafanyakazi wanaostahili kisheria, ili kulinda haki na ustawi wa wafanyakazi hao.

Mbunge wa Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu leo Februari 26, 2026 anaendelea na ziara yake katika kata ya Tendomuze, Sumbawanga Mjini, Kata ya Kaengesa na kata ya kanda.