Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Sangu: Kampuni za huduma migodini zisajiliwe OSHA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amewaagiza menejimenti za migodi nchini kuhakikisha makampuni yanayotoa huduma katika mgodi (Sub Contractors) kusajiliwa OSHA ili kutekeleza kikamilifu matakwa ya Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.


‎Aidha, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda maisha ya wafanyakazi na kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa salama, hususan katika sekta ya madini ambayo inahusisha vihatarishi vingi vya kiafya na kiusalama.

Waziri amesema hayo Februari 21, 2026 wakati wa ziara yake katika Mgodi wa Dhahabu Geita GGM ambayo ililenga la kukagua shughuli za kazi katika mgodi huo, kusikiliza changamoto zao na kujionea namna mgodi huo unavyotekeleza Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na sheria nyingine za kazi.

‎Kwa upande mwengine, Waziri Sangu amewataka waajiri na wamiliki wote wa maeneo ya kazi nchini ambao bado hawajajisajili OSHA, kuhakikisha wanasajili maeneo yao ya kazi OSHA ndani ya miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, 2026, akisisitiza kuwa muda huo ni wa mwisho kwa utekelezaji wa agizo hilo.

‎Vilevile, amewapongeza OSHA kwa kaguzi wanazofanya katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini ambazo zimekuwa na tija katika kuhakikisha waajiri wanazingatia sheria na kuweka mifumo madhubuti ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kusababishwa na mazingira hatarishi ya kazi. Pia, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, katika shabaha 12, ambapo shabaha ya nane inalenga kinga ya jamii, ikiwamo dhana ya usalama mahali pa kazi.

‎"OSHA imekuwa ikitekeleza wajibu wake wa msingi kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kuandaa na kusimika mifumo ya usalama, hatua inayochangia kulinda nguvu kazi ya Taifa," amesema

‎Kadhalika, Waziri Sangu ameipongeza GGM kwa mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa, kuboresha ustawi wa wafanyakazi wake na wananchi wanaozunguka migodi hiyo, pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza fursa za ajira.