Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Sekta ya Kilimo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi: Mhe. Katambi


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema sekta ya kilimo ina mchango mkubwa kwenye maendeleo ya ukuaji wa uchumi nchini.

Mhe. Katambi amebainisha hayo Agosti 8, 2023 wakati wa kilele cha sherehe na siku kuu ya Wakulima (nane nane) kanda ya kati katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.

Amesema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo, uvuvi na ufugaji kwa ustawi wa maisha yao.

Aidha, Mhe. Katambi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka dhamira ya dhati kuhakikisha inaimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo na mifugo kupitia mfumo wa ruzuku.

Kwa upande mwengine, Naibu Waziri Katambi amezitaka halmashauri na mashirika ya umma na binafsi yanayoshughulika na kilimo kuweka mipango ya kuwasajili wakulima ili wanufaike na fursa ya kutumia ruzuku za serikali.

Pia, ametoa wito kwa taasisi za kifedha kukopesha vijana, wanawake na Watu wenye Ulemavu wanaojishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi ili waweze kupata mitaji ya kuendeleza shughuli hizo.

Maonesho na Sherehe za Nanenane Mwaka 2023 yalikuwa na kaulimbiu isemayo “VIJANA NA WANAWAKE NI MSINGI IMARA YA MSINGI IMARA WA MIFUMO ENDELEVU YA CHAKULA”.