Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali inafanya uchambuzi mkataba wa wafanyakazi majumbani


BUNGE limeelezwa kuwa katika mwaka 2023/24, Serikali imeanza hatua ya uchambuzi wa Mkataba namba 189 wa wafanyakazi wa majumbani kwa kupitia Sheria na Kanuni zinazosimamia wafanyakazi hao.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Patrobas Katambi ameyasema hayo Novemba mosi, 2023 bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mhe. Dkt. Thea Ntara ambaye amehoji lini serikali itathibitisha mkataba huo.

Akijibu swali hilo, Mhe.Katambi amesema baada ya hatua ya mapitio kukamilika, hatua inayofuata ni ya kushirikisha wadau kwa lengo la kupokea maoni yao kuhusu maeneo ambayo serikali inapendekeza kuridhia katika Mkataba husika.

Aidha, amesema serikali itazingatia umuhimu wa vipengele vya mkataba ambavyo vitazingatia mila, desturi na uwezo wa nchi katika kutekeleza Mkataba husika.

Awali, amefafanua kuwa hatua ya kuridhia mkataba huo ilianza mwaka 2011 hadi 2016 ambapo ulifika hatua ya kuridhiwa kwa kuwasilishwa Bungeni.

Hata hivyo, amesema kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi na utekelezaji wa mkataba tajwa, iliamuliwa kuwa wadau waendelee kupewa elimu kuhusu Mkataba huo kabla ya hatua za uridhiaji kuendelea.

“Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani CHODAWU imetoa elimu kuhusu Mkataba husika kupitia Makongamano na vikao 90 ambao ni wafanyakazi wa majumbani, Viongozi wa vyama vya wafanyakazi na waajiri,”amesema