Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali Itasimamia Mkandarasi wa SGR Kulipa Madeni ya Michango NSSF: Prof. Ndalichako


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema serikali itasimamia mkandarasi wa ujenzi wa reli ya SGR kulipa madeni ya michango ya wafanyakazi kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Prof. Ndalichako ameyasema hayo bungeni Novemba 10, 2023 alipokuwa akitoa majibu ya nyongeza kwenye swali la Mbunge wa Maswa Magharibi Mhe.Mashimba Ndaki aliyetaka kujua kauli ya serikali kuhusu malalamiko ya mkandarasi huyo kuchelewesha michango NSSF.

Akijibu swali hilo, Mhe. Waziri Ndalichako amesema ni kweli mkandarasi huyo anadaiwa na tayari wameingia makubaliano na NSSF kulipa michango hiyo ndani ya mwaka mmoja.

“Nalitaarifu Bunge kuwa kuna utaratibu umewekwa NSSF na mkandarasi kwa wale ambao wanatakiwa kulipa mafao yao sasa kuna utaratibu maalum wa fedha zao kupatikana ili wasiathirike na malipo hayo,” amesema

Amelihakikishia Bunge kuwa Ofisi hiyo ambayo ina dhamana ya kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii itafuatilia madeni hayo ili haki za wafanyakazi zisipotee.