Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali yaanza Mapitio ya Sera ya Watu wenye Ulemavu


OFISI ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeanza kufanya tathmini na mchakato wa mapitio ya Sera ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 ili kukidhi mahitaji ya sasa.

Akifungua kikao cha wadau Agosti 24, 2023 jijini Dodoma cha kupitia taarifa ya awali ya mapitio hayo, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof.Jamal Katundu, amesema mapitio hayo yanafanywa na serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake(UN WOMEN) huku akitaka yazingatie uwakilishi wa makundi yote ya Watu wenye Ulemavu ili kuwa na sera bora.

Naye, Mwakilishi wa UN WOMEN, Jacob Kayombo, amesema shirika limeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya mchakato huo na kwamba wanaamini itakamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Jonas Lubago, ameishukuru serikali kwa kutimiza ahadi ya kufanya maboresho ya sera hiyo na kuahidi kushiriki kikamilifu ili kuwa na maboresho mazuri ya sera.

Awali, Mshauri Elekezi ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Consolata Sulley, amesema katika hatua ya awali ya mapitio utafanyika utafiti kwa kupata maoni kutoka kwa wadau ili kuwa na sera bora inayozingatia haki na masuala ya kijinsia kwa Watu wenye Ulemavu.