Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali yapaisha Ustawi wa watu wasioona nchini


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi, amebainisha kuwa serikali kupitia Mwongozo wa Viwango vya Vifaa vya TEHAMA wa mwaka 2020 umejumuisha mahitaji ya watu wasioona ili kuweka mazingira rafiki kwenye Ofisi za Umma na maeneo ya kutolea huduma kwa Wananchi.

Ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Watu wasioona Kitaifa yaliyofanyika Babati Mjini, Mkoani Manyara leo tarehe 21 Oktoba, 2022.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Ujumuishwaji wa Watu Wasioona katika Ajira, Michezo na Tehama kwa Maendeleo Endelevu”.

Amebainisha kuwa serikali imeendelea kutoa Ajira kwa Watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye ulemavu wa kutoona ambapo kwa mwaka 2022 Ajira zilizotolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI za Kada ya Walimu nafasi 9,800 na Kada za Afya 7,612 jumla ya Watu wenye Ulemavu 261 sawa na 2.7% walikidhi vigezo na kupata ajira ya ualimu,

“Kati ya hao 261 Watu wasioona walikuwa 61 (Ke. 13 na Me.49). iIlevile, kwa upande wa Kada za Afya jumla ya Watu wenye Ulemavu 42 walikidhi vigezo na kupata ajira ambapo miongoni mwao wasioona walikuwa wanne (4) Ke. 1 na Me.3”

Mhe. Katambi amefafanua kuwa serikali ya Mhe. Rais Samia inatambua na kutoa kipaumbele kwa masuala ya Watu wenye Ulemavu, ambapo tayari imezindua Mwongozo wa Taifa wa Utambuzi wa Mapema na Afua Stahiki kwa Watoto wenye Ulemavu.

“Lengo kuu la kuzindua mwongozo huu ni kusaidia kuwatambua Watoto wenye ulemavu na kusaidia kuweka mipango mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya ili kuwapunguzia makali ya ulemavu na pengine kuuondoa kabisa”

Aidha, Mhe. Katambi ameongeza kuwa Serikali imeona ipo haja ya kuhakikisha Watoto wenye ulemavu wanapata elimu kama Watoto wengine wasio na ulemavu na hivyo kutunga Sera ya Elimu Jumuishi, hii ni hatua ya kuhakikisha kuwa Watoto wenye ulemavu wa kawaida wanaweza kupata elimu pamoja na watoto wengine katika maeneo yao.