Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali Yapongezwa kwa Kuimarisha Ustawi wa Wafanyakazi


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imepongezwa kwa kuendelea kuimarisha ustawi wa wafanyakazi wanaopata madhira kazini kwa kuwalipa fidia zinazotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe.Fatuma Toufiq ametoa kauli hiyo Oktoba 18, 2023 jijini Dodoma kwenye kikao cha kamati hiyo na menejimenti ya WCF cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo, mafanikio na mikakati ya kukabiliana na changamoto.

“Serikali inafanya kazi nzuri sana, tunatambua juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi kwa madhara wanayoyapata kazini, kamati inalitambua hilo na tutaendelea kuishauri serikali ikiwezekana bajeti iongezeke na kuimarisha zaidi ustawi wa wafanyakazi ili wanaoumia kazini wapate stahiki zao. Tunasisitiza elimu zaidi itolewe kwa wananchi kuhusu mfuko huu,”amesema.

Naye, Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, ameihakikishia kamati kuwa WCF itaendelea kutoa elimu kwa umma ili kupata huduma zinazostahili wanapopata madhira yeyote wakiwa kazini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Patrobas Katambi, amesema kwa mujibu wa sheria kila taasisi ambayo inaajiri inapaswa kujisajili WCF na lengo la mfuko ni kusajili wanachama 3,000 kwa mwaka.

Aidha, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja,ameiahidi kamati kuwa Ofisi hiyo itaendelea kuisimamia WCF kuzingatia ushauri na maoni ya kamati hiyo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, amesema kwa mwaka 2022/23 madai 4,306 yalichakatwa na kutoa mafao yenye thamani ya Sh.Bilioni 17.9 na imechangiwa na kuongezeka kwa uelewa kwa jamii.