Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

​Serikali Yasisitiza Umuhimu wa Michezo kwa Wafanyakazi


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Rahma Kisuo, ametoa wito kwa taasisi zote za umma na binafsi nchini kutambua umuhimu wa michezo na kuhakikisha wafanyakazi wanashiriki kikamilifu.

Mheshimiwa Kisuo ametoa wito huo leo, Aprili 20, 2026, alipofungua Michezo ya Mei Mosi Kitaifa kwa mwaka 2026 iliyofanyika mkoani Njombe katika viwanja vya Sabasaba.

Amesema michezo ni msingi wa afya bora, akibainisha kuwa afya ya mfanyakazi ni mtaji mkubwa unaochochea maendeleo ya taasisi na Taifa kwa ujumla.

Aidha, amewahimiza wafanyakazi kote nchini kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, akisisitiza kuwa mazoezi yasifanywe wakati wa mashindano pekee bali yawe sehemu ya maisha ya kila siku.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Kisuo amewapongeza washiriki wote wa michezo hiyo na kuwaasa kuzingatia nidhamu, mshikamano pamoja na ushindani wa haki. Amesisitiza kuwa michezo inapaswa kuwa chachu ya kuimarisha udugu miongoni mwa wafanyakazi na si chanzo cha migogoro.

Kwa mwaka 2026, Michezo ya Mei Mosi inaongozwa na kauli mbiu isemayo:

“Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”