Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Serikali Yazindua Programu na Mkakati Wa Kazi Za Staha


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu amezindua Programu ya Nchi ya Kazi za Staha Awamu ya Tatu ya Mwaka 2025/2026 – 2029/2030 na Mkakati wa kukuza Kazi za Staha Kwa wafanyakazi wa nyumbani.

Aidha, amesema Progamu hii inalenga kuimarisha majadiliano ya kijamii na mshikamano baina ya Serikali, Waajiri, Wafanyakazi na wadau mbalimbali. Ameongeza kuwa mshikamano huo ni msingi wa kujenga uchumi shindani na endelevu.

Uzinduzi huo umefanyika leo Februari 13, 2026 katika ukumbi wa Hoteli ya Best Western, Jijini Dodoma.

Vilevile, Waziri Sangu amesema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayo rahisisha utekelezaji wa programu hiyo ili kukuza maendeleo kupitia kazi za staha.

"Tanzania ni Taifa linalojali utu, haki, mshikamano hivyo kuwa na kazi za staha ni msingi wa maendeleo ebdelevu," amesema

Pia, Waziri Sangu ameshukuru ILO kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kisera, programu, miongozo, mafunzo na miradi.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Kazi, Suzan Mkangwa amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuridhia mkataba wa wafanyakazi wa majumbani, hivyo kukamilika wa Programu ya Nchi ya Kazi za Staha Awamu ya Tatu utasaidia kufanikisha maridhiano ya mkataba huo.

Kadhalika, Kamishna Mkangwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuwapatia kipaumbele wafanyakazi wa nyumbani kwa kusimamia maslahi yao na kuwalinda kupitia mifumo ya sheria ikiwemo Sheria ya Mahusiano Kazini ambayo inaainisha viwango vya kazi wote ikiwa ni Pamoja na wafanyakazi wa nyumbani.

Naye, Mkurugenzi Shirika la Kazi Duniani (ILO) Afrika Mashariki, Bi. Caroline Mugala, amesema kazi za staha ni utu hivyo jambo jema nchi wanachama wa ILO kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi za staha kwa kuwa zinahakikisha haki katika maeneo ya kazi, kinga ya jamii na majadiliano mema katika maeneo ya kazi.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa programu ya kazi za staha itaimarisha Maendeleo ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania.