News
Soko la Ajira Kidijital
Waajiri kutoka Sekta Binafsi wamefurahishwa na kuipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Wazifri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kwa kuanzisha Mfumo wa Taifa wa Kielektroniki wa Taarifa za Soko la Ajira (NLMIS) wakieleza kuwa hatua hiyo ni mageuzi makubwa katika usimamizi na upatikanaji wa taarifa sahihi za Ajira nchini.
Wamesema mfumo huo utawarahisishia kupata takwimu na taarifa za Ajira zinazozalishwa kwa haraka na kwa wakati, hivyo kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu mahitaji ya rasilimali watu kulingana na mwelekeo wa soko.
Akizungumza Februari 25, 2026, Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala wa Power Group Technologies Tanzania Limited Salha Irando, amesema Mfumo huo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika uandaaji wa mikakati na mipango inayohusu taarifa za soko la ajira kwa usahihi na ufanisi .
Naye, Mkuu wa Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Bakharesa Group Francis Ndenje amesema mfumo huo utasaidia katika upatikanaji wa takwimu sahihi na za wakati utakaowezesha taasisi kupanga mahitaji ya rasilimali watu kulingana na mwenendo halisi wa soko la ajira nchini.
Akizungumza awali, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Godwin Mpelumbe, amesema Serikali ina matarajio makubwa kwa waajiri kushiriki kikamilifu kutoa taarifa sahihi za ajira zinazozalishwa katika taasisi zao.
Mfumo wa Taifa wa Kielektroniki wa Taarifa za Soko la Ajira unatarajiwa kuongeza uwazi na ushindani wa haki katika mchakato wa ajira, huku ukiimarisha ushirikiano kati ya Serikali, waajiri na taasisi za mafunzo. Hatua hii inaonesha dhamira ya Serikali ya kutumia teknolojia kama nyenzo muhimu ya kukuza ajira, kuongeza tija, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
