News
Tanzania Kuratibu Mkutano wa Nchi za Ghuba
Tanzania inatarajia kuratibu Mkutano wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (Doha Dialogue) mwezi Oktoba mwaka huu, kama sehemu ya juhudi za kuendelea kukuza fursa za ushirikiano katika ukuzaji wa ajira na kazi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu, mara baada ya kukutana na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Mheshimiwa Fahad Rashid Al-Marekhi, leo Aprili 20, 2026, katika Ukumbi wa Benjamin Mkapa Tower, Dar es Salaam.
Waziri Sangu alisema lengo la kikao hicho ni kujadili maandalizi ya Mkutano wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba pamoja na nchi za Afrika, wenye lengo la kuongeza fursa za ajira na kuimarisha mahusiano ya kikazi. Mkutano huo unapangwa kufanyika tarehe 5 hadi 6 Oktoba 2026 nchini Tanzania.
Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC) linahusisha nchi za Qatar, Oman, Saudi Arabia, Falme za Nchi za Kiarabu (UAE) pamoja na nchi za Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya na Ethiopia.
Awali akizungumza Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Fahad Rashid Al-Marekhi, alieleza kuwa nchi yake inaunga mkono kikamilifu juhudi za Tanzania katika kuratibu mkutano huo muhimu, akisisitiza kuwa Doha Dialogue ni jukwaa la kimkakati linalolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiteknolojia kati ya nchi za Ghuba na Afrika.
Alibainisha kuwa Qatar inaona Tanzania kama mshirika muhimu katika ukanda wa Afrika Mashariki, hasa katika maeneo ya uwekezaji, ajira na maendeleo ya rasilimali watu.
Aidha, Balozi Al-Marekhi alisisitiza utayari wa Qatar kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika maandalizi ya mkutano huo ili kuhakikisha unakuwa na mafanikio makubwa na tija kwa pande zote. Aliongeza kuwa kupitia mkutano huo, fursa mpya za ajira, ubadilishanaji wa ujuzi na uwekezaji zitaimarishwa, hatua itakayochangia kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wa mataifa husika.
