Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Thamani ya Mfuko wa NSSF yafikia Trilioni 11.2



✅ Waziri Sangu Abainisha Hifadhi Skimu Inavyoenda Kubadili Maisha ya Watanzania

Na: Mwandishi Wetu - Dodoma

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kuimarika kwa kasi, ukifikia thamani ya shilingi trilioni 11.2 hadi Machi 2026 kutoka trilioni 4.3 mwaka 2020, hatua inayoakisi ukuaji wa uwekezaji, uimara wa usimamizi na kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi kupitia Hifadhi Skimu.

Ukuaji huo umeambatana na upanuzi wa huduma za hifadhi ya jamii, hususan kupitia hifadhi skimu zinazolenga kuwafikia wananchi waliojiajiri, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza wigo wa wanachama na kuimarisha ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ya jamii katika mfumo wa hifadhi ya jamii.

Akizungumza jijini Dodoma tarehe 27 Aprili 2026 wakati akifungua Mkutano wa 56 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, alisema mafanikio ya Mfuko yanatokana na mageuzi ya usimamizi, uwekezaji wenye tija na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

Alisisitiza kuwa hifadhi skimu ni nguzo muhimu ya mustakabali wa hifadhi ya jamii nchini, akibainisha kuwa Serikali inalenga kuhakikisha Watanzania wengi zaidi, hususan waliojiajiri, wanajumuishwa katika mfumo huo.

"Upanuzi wa hifadhi skimu ni hatua muhimu ya kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nje ya mfumo wa hifadhi ya jamii," alisema Mhe. Sangu.

Waziri huyo pia aliipongeza NSSF kwa mchango wake katika uchumi wa taifa kupitia uwekezaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayozalisha ajira na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi, akitaja kiwanda cha sukari cha Mkulazi kuwa mfano wa uwekezaji wenye tija.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema mafanikio hayo yametokana na usimamizi madhubuti wa fedha, uwekezaji salama na matumizi ya mifumo ya TEHAMA iliyofikia takribani asilimia 99 ya huduma.