News
Thamani ya mfuko WCF yafikia TZS 844.41Bilioni,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amepongeza jitihada zinazofanywa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika kutekeleza majukumu yake, hatua iliyochangia ukuaji wa Mfuko huo na kufikia thamani ya TZS 844.41Bilioni, Mwezi Desemba 2025 kutoka TZS 333.46 Bilioni, Mwezi Juni 2020.
Amesema mafanikio hayo yameufanya Mfuko kuwa imara zaidi na wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa mujibu wa Ripoti ya Tathmini ya Mifuko iliyofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2022.
Mhe. Sangu ameyasema hayo Februari 18, 2026 mjini Morogoro wakati akifungua Mkutano wa Tano wa Baraza la Tatu la Wafanyakazi wa WCF, ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kupokea na kujadili mpango wa bajeti ya Mfuko kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji wenye tija uliofanywa na Mfuko katika maeneo mbalimbali, ikiwemo hati fungani za Serikali, makampuni binafsi, uwekezaji katika ardhi, hisa katika masoko ya mitaji, amana za benki pamoja na uwekezaji wa pamoja.
“Ukuaji wa thamani ya WCF umetokana na uwekezaji wenye tija uliofanywa na Mfuko, ambapo hadi kufikia Desemba 2025 thamani ya uwekezaji imeongezeka na kufikia TZS 891.12 Bilioni, Haya ni mafanikio makubwa ambayo kwa namna moja ama nyingine Baraza hili limechangia,” amesema Mhe. Sangu.
Aidha, ameongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, WCF imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kukusanya michango kutoka kwa waajiri na kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaopata madhira wanapokuwa kazini. Hadi kufikia Desemba 2025, jumla ya waajiri 44,834 walikuwa wamesajiliwa na Mfuko, huku zaidi ya TZS 124 Bilioni, zikitumika kulipa fidia kwa wafanyakazi waliopata madhira kazini.
Vilevile, Mhe. Sangu ametoa maelekezo kwa uongozi wa WCF kuhakikisha haki za msingi za wafanyakazi zinazingatiwa, ikiwemo kupandishwa vyeo kwa wakati, kupata likizo, mafunzo pamoja na motisha mbalimbali kwa uwazi na bila upendeleo. Pia amewataka wajumbe wa Baraza kuhakikisha wafanyakazi wanashirikishwa ipasavyo katika mipango ya Mfuko na kuhimiza uwajibikaji, ambao ni nguzo muhimu ya mafanikio katika sehemu yoyote ya kazi.
