News
Waajiri wakumbushwa wajibu wa kuripoti Ajali Kazini
Na: OWM (KAM) - Njombe
WAAJIRI nchini wamekumbushwa kuzingatia kikamilifu wajibu wao wa kisheria wa kuripoti matukio ya ajali yanayotokea mahali pa kazi, kwa mujibu wa Kifungu Na. 101 cha Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, Sura Namba 297, Toleo la mwaka 2023 ili kuiwezesha Taasisi ya OSHA kufanya uchunguzi wa kina na kubaini vyanzo vya ajali katika maeneo ya kazi na kisha kushauri njia madhubuti za kuzuia matukio ya ajali kujirudia.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu leo 28 Aprili, 2026 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema, Mkoani Njombe ambapo amesisitiza kuwa utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu ajali kazini ni hatua muhimu katika kulinda afya na usalama wa wafanyakazi pamoja na kuimarisha mazingira bora ya kazi.
Mhe. Sangu amesema kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kitaifa, ripoti za ukaguzi wa OSHA na takwimu za fidia kwa wafanyakazi zinaonyesha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha majeraha na vifo vinavyotokana na kazi. Ameeleza kuwa, Utafiti wa mwaka 2025 katika viwanda vya chuma na bidhaa za chuma ulionyesha kuwa asilimia 65.1 ya wafanyakazi hupata majeraha kazini kila mwaka. Takribani asilimia 64.6 ya wafanyakazi waliojeruhiwa walihitaji kulazwa hospitalini au kutofika kazini kwa muda.
“Waajiri kuripoti ajali kunaiwezesha taasisi ya OSHA kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tukio husika, hatua itakayosaidia kutoa mapendekezo sahihi ya namna ya kuzuia ajali kama hizo zisijirudie siku zijazo na hivyo kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kwa wafanyakazi,” amesema
Vile vile, amesema jitihada za Serikali katika kuimarisha masuala ya usalama na afya kazini zimejidhihirisha katika Dira ya Taifa ya mwaka 2050 kupitia nguzo ya kwanza inayosisitiza juu ya kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani ambayo utekelezaji wake umeanza. Aidha, Waziri Sangu amesema OSHA inatekeleza programu ya Afya Yangu-Mtaji Wangu ambapo kupitia programu hiyo makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo wakiwemo mafundi wa kada mbalimbali, makundi ya watu wenye ulemavu, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya kati na vyuo vikuu na wachimbaji wadogo yamefikiwa.
Kwa upande mwengine, Mhe. Sangu amewataka waajiri wote nchini ambao hawajasajili maeneo yao ya kazi OSHA kuhakikisha wanasajili maeneo yao kabla ya kuanza kwa kampeni maalum ya kufuatilia utekelezaji wa agizo husika ambapo ufuatiliaji huo utaambatana na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kuendesha shughuli za uzalishaji bila kutambuliwa na OSHA.
Akizungumza awali, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka, ameishukuru OSHA kwa kuandaa na kuadhimisha Wiki ya Usalama na Afya katika Mkoa wa Njombe. Amesema maadhimisho hayo yamefungua fursa kwa wakazi wa mkoa huo pamoja na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi na kunufaika na huduma mbalimbali zilizotolewa kupitia maonesho hayo.
Naye Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mary Maganga amemhakikishia Mheshimiwa Waziri kuwa wataendelea kusimamia Sheria, Sera ba Miongozo kuhusu usalama na afya inafuatwa na waajiri kwa lengo la kuweka mazingira salama kwa wafanyakazi wao.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu waOSHA, Khadija Mwenda amesema Taasisi hiyo itaendelea kusimamia uwepo wa mazingira ya usalama na afya katika maeneo ya kazi ili kuendendela kujenga uchumi imara nchini.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewata wafanyakazi kutoa taarifa endapo wataona viashiria hatarishi katika maeneo yao ya kazi ili hatua Madhubuti za kuzuia madhara ziweze kuchukuliwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Doran, mewasihi waajiri nchini kuzingatia kikamilifu na kutekeleza Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa kuhakikisha wanajenga na kuimarisha mifumo madhubuti ya usalama kazini. Amesema ni muhimu kwa waajiri kuweka mazingira salama yanayolinda si tu usalama wa kimwili wa wafanyakazi, bali pia ustawi wao wa kisaikolojia, kama sehemu ya msingi ya usimamizi bora wa biashara. Pia, amesisitiza utamaduni wa kinga kwanza, ili kupunguza ajali na kuimarisha tija mahali pa kazi.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa nchi za Afrika Mashariki Caroline Mugalla amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama na yenye afya njema kwa wote.
MWISHO
