News
Wachimbaji Bukombe watakiwa kuzingatia usalama kazini
Serikali imewataka wachimbaji wadogo wilayani Bukombe mkoani Geita kuzingatia masuala ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ili kuepuka ajali na magonjwa yanayoweza kuhatarisha maisha yao na kuathiri uzalishaji.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Usalama na Afya kazini yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Februari 21, 2026 Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuhimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.
Akizungumzia mafunzo hayo, amesema kuwa tangu asubuhi wakufunzi kutoka OSHA wamekuwa wakitoa elimu kwa wachimbaji hao kuhusu vihatarishi vinavyowazunguka katika shughuli zao za uchimbaji madini.
“Vihatarishi hivi visipodhibitiwa vinaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo ajali na magonjwa ya kazini. Nina imani kila mmoja wenu ameelewa wajibu wake wa kuchukua tahadhari,” amesema.
Aidha Waziri Sangu ameupongeza uongozi wa OSHA chini ya Mtendaji Mkuu, Bi. Khadija Mwenda, kwa kuona umuhimu wa kuwafikia wachimbaji wadogo kwa mafunzo hayo, huku akibainisha kuwa yamegharamiwa na Serikali kama sehemu ya jitihada za kulinda makundi yote ya wafanyakazi.
Ameongeza kuwa mbali na mafunzo ya utambuzi wa vihatarishi, wachimbaji hao pia wamepata mafunzo ya huduma ya kwanza ili kuwawezesha kutoa msaada wa awali endapo ajali itatokea kabla ya majeruhi kufikishwa hospitalini.
Vile vile ametoa rai kwa wachimbaji kuendelea kuchukua tahadhari binafsi na kutumia vifaa kinga wanapotekeleza shughuli zao ili kuepuka madhara yanayoweza kuzuilika.
“Huwezi kuzungumzia uchumi bila kuzingatia usalama na afya. Vitu hivi vinaenda sambamba. Mfanyakazi ndiye msingi wa uzalishaji. Akipata ajali au kuugua, uzalishaji unasimama na familia pamoja na taifa hupata hasara,” Amesema.
