News
Wachimbaji wadogo wa Madini wahimizwa kuchangamkia fursa za Mkopo unaotolewa na Serikali
Wachimbaji wadogo wa madini wamehimizwa kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na serikali ikiwemo wa Mfuko wa maendeleo ya Vijana unao ratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuanzisha au kuimarisha shughuli zao za uzalishaji mali.
Wito huo umetolewa Julai 3, 2025 na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Daudi Silasi wakati mafunzo ya kuwaongezea ujuzi wachimbaji wadogo wa Madini mkoani Geita.
Amesema, Mikopo hiyo inatolewa mahsusi kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwa tija, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali ya awamu ya sita za kupunguza ukosefu wa ajira na kukuza uchumi wa wananchi.
“Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeweka mazingira rafiki kwa vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa. Tunawahimiza wachimbaji wadogo, hasa vijana, kujiunga katika vikundi, kuandaa maandiko ya miradi na kuwasilisha ofisini, mkikidhi vigezo mtapewa fedha kulingana na ukubwa wa mradi” amesema.
Akizungumza mchimbaji mdogo wa madini Hellen Josephat ametoa shukrani kwa serikali kwa kuendelea kuwajali wachimbaji wadogo kwa kuwapatia elimu na fursa za mikopo zinazotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Naye, Alphonce Daniel ameishukuru serikali kwa kutoa mafunzo na elimu kuhusu fursa za mikopo na ujasiriamali kwa wachimbaji wadogo ambapo amesema kupitia mafunzo hayo, ameelewa umuhimu wa kujiunga katika vikundi, kuandaa maandiko ya miradi na kufuata taratibu sahihi za kisheria ili kupata mkopo.
Lengo la kuanzishwa kwa Mfuko huo ni kuwawezesha vijana kiuchumi kwa njia ya kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu. Mikopo hii humsaidia Kijana mmoja mmoja au vikundi vya uzalishaji mali, kupata mitaji kwa ajili ya kuimarisha au kuanzisha miradi mipya ya kiuchumi inayowawezesha kupata kipato na hivyo kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe.