News
Wafanyakazi Waliopoteza Ajira Kulipwa Mafao Ndani ya Siku 90
Serikali imeendelea kuboresha Mifumo ya Hifadhi ya Jamii nchini kwa kufanya maboresho ya kanuni za ulipaji wa mafao ili kuongeza ulinzi na ustawi wa wafanyakazi wanaopoteza ajira wakiwa kazini.
Hayo yamebainishwa Mei 8, 2026 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Dkt. Evaline Wilbard Munisi wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Mhe. Ado Shaibu Ado, lililohoji kauli ya serikali juu ya Fao la kujitoa kwa Waajiriwa na lini Serikali inafikiria kuanzisha Fao hilo.
Akijibu swali hilo, Dkt. Munisi amesema Serikali imefanya maboresho ya kanuni za fao la kukosa Ajira ili kumpa mwanachama uchaguzi wa namna ya kunufaika baada ya kupoteza ajira ambapo mtumishi sasa anaweza kuamua kulipwa mkupuo maalumu au kuendelea kulipwa asilimia 33.3 ya mshahara wake kwa kipindi cha miezi sita. Utaratibu huo unaolenga kumwezesha kuendelea kuwa na sifa za kupata pensheni atakapostaafu.
Amesema maboresho hayo yanaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha watumishi wanaopoteza Ajira wanapata kinga ya kiuchumi bila kuathiri mafao yao ya muda mrefu ya uzeeni.
Sambamba na hayo Dkt. Munisi ameeleza kuwa Serikali tayari imesaini kanuni mpya mwaka 2025 zinazomruhusu Mwajiriwa aliyepoteza Ajira kulipwa mafao yake kwa mkupuo ndani ya siku tisini tangu kupoteza ajira hiyo.
Katika mifuko ya hifadhi ya jamii hakuna fao la kujitoa kwa mwanachama anapopoteza ajira, bali kinachotambuliwa kwa sasa ni fao la kukosa ajira lililoboreshwa mwaka 2025 ili kuendana na mahitaji ya wafanyakazi na hali ya soko la ajira nchini. amesema.
Hatua hiyo ya Serikali inaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na kuhakikisha wafanyakazi wanapata usalama wa kipato wanapokumbwa na changamoto ya kupoteza ajira.
MWISHO
