Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAJUMBE WA BARAZA LA WAFANYAKAZI OFISI YA WAZIRI MKUU WAHIMIZWA KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA UFANISI


Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wamehimizwa kutekeleza majukumu kwa ufanisi na weledi ili kuimarisha utendaji kazi wao.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde ametoa kauli hiyo hii leo Jijini Arusha alipokuwa akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo uliyofanyika katika ukumbi wa Mkutano uliyopo katika hoteli ya Gold Crest, Machi 8, 2020.

Alieleza kuwa uwepo wa Baraza la Wafanyakazi katika sehemu za kazi unasaidia kuongeza ushirikishwaji wa watumishi katika kupanga na kutekeleza majukumu yao, kuleta usawa katika kujadili mambo muhimu, kutoa ushauri juu ya tija na ufanisi wa kazi ikiwemo kukumbushana, kuelimishana na kuweka mazingira bora ya utendaji kazi na kuweka umoja kati ya wafanyakazi na viongozi.

“Ni matumaini yangu Baraza hili litakuwa na mijadala yenye uwazi na mambo yote yatakayojadiliwa yatasaidia kuimarisha utendaji wa majukumu ya Ofisi kwa lengo la kuhakikisha mazingira ya utendaji kazi yanaboreshwa kwa manufaa ya kutoa huduma bora kwa wananchi, inajulikana kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ina mambo mengi yanayogusa jamii moja kwa moja na hasa masuala ya Kazi, Ajira, maendeleo ya vijana na watu wenye ulemavu,” alisema Mavunde.

Aliongeza kuwa ni muhimu kwa kila mjumbe wa Baraza hilo kutumia nafasi aliyopewa ili uwakilishi wake uweze kuleta tija na kuwa chachu katika kuleta maendeleo ya watumishi wote kwa ujumla.

Sambamba na hayo Naibu Waziri Mavunde alitoa maagizo kwa Wajumbe wa Baraza ikiwemo suala la kusimamiwa vizuri sekta ya kazi hususani kuongezwa jitihada za zaidi katika kufanya kaguzi mara kwa mara ili kuhakikisha sheria na kanuni za kazi hapa nchini zinafuatwa.

Pia alitilia mkazo juu ya matumizi ya teknolojia katika kuwahudumia wananchi kwa haraka na wepesi, hivyo alihimiza Baraza hilo kuandaa mpango endelevu utakao wawezesha watumishi kujifunza matumizi ya teknolojia mpya ambayo ni dhabiti katika kutoa huduma.

Aidha, Mheshimiwa Mavunde alitoa wito kwa kila mjumbe wa baraza hilo kushirikiana na watumishi wenzao na wote kwa pamoja watambue kuwa wanao wajibu wa kufanikisha malengo ya Serikali na Ofisi hiyo.

Halikadhalika aliwasihi wajumbe wa baraza hilo kuendelea kutekeleza taratibu na sheria za kupambana na masuala ya rushwa katika maeneo ya kazi. Pamoja na hayo alipongeza utendaji wa watumishi wa ofisi yake kwa utekeleza wa majukumu mbalimbali ikiwemo ubunifu katika kuratibu programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, kwa lengo la kulinda mazingira ya kazi na ajira nchini, kuanzishwa kwa mfumo wa kielektroniki wa vibali na uratibu wa mfuko mfuko wa maendeleo ya Vijana ambao unawezesha vijana kiuchumi.

Awali wakati wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo la Wafanyakazi alisema kuwa majadiliano ambayo yamekuwa yakifanyika katika mkutano wa baraza hilo yamekuwa yakisaidia kutatua changamoto zinazojitokeza sehemu ya kazi na pia kuboresha mazingira ya utendaji na kazi.