News
Watumishi wapya Ofisi ya Waziri Mkuu waahidi uzalendo
Waajiriwa wapya katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira na Mahusiano wamesema kuwa mafunzo elekezi waliyopata kwa siku tano yamewapa uelewa mpana na mwelekeo sahihi wa namna ya kuutumikia umma kwa ufanisi.
Wameeleza kuwa mafunzo hayo waliyopata yatawasaidia kukabiliana na changamoto za kazi, kufanya maamuzi sahihi, na kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu kwa weledi na uzalendo.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu,Ajira na Mahusiano Mary Maganga, Kamishna wa Kazi Msaidizi toka Ofisi hiyo alisema jumla ya wammwatumishi wapya 40 walioajiriwa kuanzia mwaka 2025 hadi 2026, wamepata mafunzo ambayo yamehitimishwa leo Februari 6, 2026 Jijini Dodoma.
Kamishna Moyo alisema mafunzo hayo ya siku tano yalilenga kuwaandaa watumishi hao kuanza rasmi utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Katika mafunzo hayo washiriki walipata elimu kuhusu haki na wajibu wa mtumishi wa umma, nidhamu kazini pamoja na umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia weledi
Kamishina Moyo aliwataka waajiriwa wapya kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, bidii na uzalendo wakizingatia kuwa wao ni sehemu muhimu ya Serikali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wao baadhi ya waajiriwa wapya walisema mafunzo elekezi ya awali yanatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa huduma ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano.
Waajiriwa wapya wameahidi kufanya kazi kwa moyo wa kujituma, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kushiriki kikamilifu katika kufanikisha malengo ya Serikali kwa manufaa ya Taifa.
