Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndalichako ashiriki Mkutano wa 111 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO)


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki katika Mkutano wa 111 wa Shirika la Kazi Duniani (ILC 111) unaofanyika jijini Geneva, Uswisi katika Makao Makuu ya Shirika hilo.

Akizungumza katika Mkutano huo tarehe 12 Juni, 2023, Prof. Ndalichako ameeleza baadhi ya masuala ambayo Tanzania imeyatekeleza katika kukuza usawa mahali pa Kazi. Amebainisha masuala hayo ni Marekebisho ya Sheria katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii ili kuongeza wigo wa Hifadhi ya Jamii katika Sekta isiyo rasmi, kutangazwa kwa kima cha chini cha mshahara na kuendelea na mapitio ya sheria za kazi ili kuimarisha utekelezaji wa Kanuni za Msingi na Haki za Kazi (Principles and Rights at Work) na kutunga Kanuni Sita zinazohusu masuala ya Afya na Usalama Pa Kazi.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kugharimia Programu za Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi kwa Vijana.

Kwa upande mwingine, Mheshimiwa Waziri amewasilisha maoni na mchango wa Tanzania katika Ripoti ya Mkurugenzi Mkuu wa ILO Bw. Gilbert Houngbo, ambayo imesisitiza nchi wanachama kukuza na kudumisha Usawa Kitaifa na Kimataifa hasa kwa makundi ya wafanyakazi ambayo yapo katika hatari kubwa ya kuathirika na aina mbalimbali za unyanyasaji.

Vile vile, Mhe. Waziri Ndalichako amesisitiza utayari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza ushirikiano na ILO pamoja na wadau wengine katika kutekeleza mikataba mbalimbali ya Shirika hilo.