Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ridhiwani Kikwete akabidhi vifaa mtaji kwa vikundi vya Vijana Wilayani Sengerema


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amekabidhi vifaa mtaji kwa vikundi vya Vijana na Watu wenye Ulemavu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 90 kwa vikundi 16 vya vijana wa wilaya ya Sengerema.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo leo Septemba 27, 2024, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kuwa vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni pamoja na vifaa vya kushonea (cherehani),Mashine ya kutotolesha vifaranga,Kompuyta,Printer, Mitungi ya gesi, Majiko na Majokofu na Mashine ya Kusaga.

Aidha, Waziri Ridhiwani amesema Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu na kusimamia afua mbalimbali za kuwezesha vijana nchini katika maeneo ya kiuchumi na kijamii ili vijana waweze kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na stadi zitakazowawezesha kufanya shughuli zitakazo waingizia kipato na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua mchango wa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa na rasilimali watu muhimu katika kukuza uchumi wa nchi,” amesema

Vile vile, Mhe. Ridhiwani ametoa rai kwa vijana wote nchini kuhakikisha kuwa wanaendelea kutekeleza wajibu wao kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa za uwezeshaji kiuchumi ili kujipatia ajira na kuweza kujitegemea.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Mhe. Senye Ngaga amemuhakikishia mheshimiwa Waziri kuwa Wilaya hiyo imejipanga kuendelea kuwezesha vijana kupitia mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye Ulemavu.

Awali akizungumza, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Eliakim Mtawa amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na UNFPA iliandaa programu mahususi kwa ajili ya vijana ambapo vijana hao walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali, uanzishaji na usimamizi wa miradi, stadi za maisha na masuala ya uongozi na usimamizi wa vikundi vya uzalishajimali.

Mwakilishi wa vikundi vya vijana vilivyonufaika, Clement Cosmas ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia kujikwamua kiuchumi.