Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Waziri Sangu aeleza dhamira ya Serikali kuboresha maslahi ya Wastaafu


✅ Asema sasa Mafao yanalipwa kwa wakati

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu ameelezea dhamira ya Serikali katika kuendelea kuboresha maslahi ya wastaafu na kuhakikisha wanapata mafao yao kwa wakati.

Mhe. Sangu ameyasema hayo Agosti 31, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Wete, Mhe. Said Ali Mbarouk aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kuondoa utaratibu wa sasa wa kikokotoo kwa Wastaafu wa Jeshi la Polisi ili kuboresha maslahi kwa Wastaafu.

Akijibu swali hilo Mhe. Sangu ameelezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuimarisha mifuko ya hifadhi ya jamii zinalenga kuhakikisha wanachama wanapata mafao yao kwa wakati pamoja na kuboresha maslahi yao.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili iweze kulipa mafao kwa wakati na kuweka mazingira ya kuboresha mafao ya watumishi katika sekta ya umma na binafsi.

Akizungumzia suala la mfumo wa kikokotoo kwa askari Polisi amesema mifuko ya hifadhi ya jamii hutumia kanuni maalum za kikokotoo katika kukokotoa na kulipa mafao kwa wanachama na wastaafu, na kwamba utaratibu huo unawahusu wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi, wakiwemo watumishi wa Jeshi la Polisi.

Vilevile, Waziri Sangu amesema kanuni hizo haziruhusu kuwepo kwa ukokotoaji tofauti wa mafao kwa wanachama wenye sifa zinazofanana ndani ya mfuko wa pensheni, hatua inayolenga kuhakikisha usawa na haki katika utoaji wa mafao.