News
Waziri Sangu ahimiza Viongozi wa Dini kulea vijana katika misingi ya uwajibikaji na uzalendo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kutumia nafasi zao kuwalea vijana katika misingi ya maadili mema, uwajibikaji na uzalendo ili kusaidia kujenga taifa lenye maendeleo endelevu.
Amesema Serikali inaendelea kufungua milango ya mazungumzo na ushirikiano na taasisi mbalimbali za dini kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya jamii na ustawi wa wananchi.
Mhe. Sangu alitoa kauli hiyo Mei 24, 2026 akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Kad Day yenye kaulimbiu ya “Mtu Bati, Bati Mtu” yaliyoambatana na Ibada ya Pentekoste kwa waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), yaliyofanyika katika viwanja vya kanisa hilo vilivyopo Kata ya Chonyonyo mkoani Kagera.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sangu alisema vijana ni nguvu kazi muhimu na msingi wa maendeleo ya taifa, jambo lililoifanya Serikali kuanzisha wizara maalum inayoshughulikia maendeleo ya vijana chini ya Ofisi ya Rais.
Vile vile Sangu alieleza kuwa Serikali pekee haiwezi kubeba jukumu la kuwalea vijana bila ushirikiano wa viongozi wa dini, familia na jamii kwa ujumla.
Aidha, aliwataka viongozi wa dini kuwafikia vijana na kuwajenga katika misingi ya maadili mema ili kuwaepusha na mmomonyoko wa maadili unaochangiwa na matumizi mabaya ya teknolojia na mazingira yasiyo salama kwa ukuaji wao.
“Viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa ya kushirikiana na Serikali katika kuwalea vijana wetu. Kundi hili linahitaji malezi bora yatakayowasaidia kuwa wananchi wenye uwajibikaji, maadili na uzalendo kwa taifa lao,” alisema Mhe. Sangu.
Katika hatua nyingine, Waziri Sangu alisema Serikali imeendelea kuwatafutia vijana ajira zenye staha kupitia fursa mbalimbali zinazopatikana ndani na nje ya nchi.
Alibainisha kuwa zaidi ya vijana 7,900 wameunganishwa na ajira katika mataifa mbalimbali, wakiwemo wauguzi na madaktari waliopata nafasi za kazi katika nchi za Uarabuni na Ujerumani, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya ajira na kuongeza kipato kwa vijana wa Kitanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahaya Ramadhan Kido, aliwakumbusha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola kutokana na mwingiliano wa shughuli za kijamii na kiuchumi na nchi jirani zilizoripoti visa vya ugonjwa huo.
Hata hivyo, Kanali Kido alisema hadi sasa Tanzania haijaripoti kisa chochote cha Ebola na kuwahimiza wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, ikiwemo kutoa taarifa mapema wanapoona dalili zinazohusiana na ugonjwa huo kupitia vituo vya afya au kwa kupiga namba ya dharura 199.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika kuimarisha amani, maadili mema na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

