News
Waziri Sangu ampongeza Rais Samia kwa kuimarisha Mifumo ya Usalama Kazini
Asema Mazingira Bora ya Kazi ni Chachu ya Tija na Utu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji Tuzo za Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (AOSH 2026) mkoani Njombe jana (29 Aprili 2026), Mhe. Sangu alisema juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita zinalenga kuhakikisha shughuli za uzalishaji nchini zinakuwa na tija huku zikizingatia utu wa watu wanaoshiriki katika uzalishaji.
Mhe. Sangu alieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na usimamizi mzuri wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, Sura Na. 297, Toleo la 2023, inayotekelezwa kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA). Alisisitiza kuwa hali hiyo imewezesha maeneo mengi ya kazi nchini kuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya.
“Mahali pa kazi panapothamini afya ya akili, usalama wa kihisia, heshima pamoja na maana ya kazi, wafanyakazi huweza kutoa mchango wao kikamilifu. Hali hiyo huongeza tija, hupunguza uchovu wa kazi na kuimarisha ubunifu,” alisema Mhe. Sangu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, alisema tuzo za AOSH hutolewa kwa lengo la kuhamasisha uzingatiaji wa viwango vya afya na usalama kazini. Alifafanua kuwa tuzo hizo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka Aprili 28.
Bi. Mwenda aliongeza kuwa maadhimisho hayo nchini Tanzania yameanza tangu mwaka 2004. Kwa mwaka huu, kauli mbiu ni: _“Mazingira Bora ya Kazi Kisaikolojia ni Njia ya Kuimarisha Ustawi wa Wafanyakazi na Kujenga Taasisi Imara.”_
Hafla hiyo ya ugawaji tuzo ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Kazini yanayoendelea mkoani Njombe kuelekea Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi.
Mwisho.
