News
Waziri Sangu Asisitiza Ushirikiano kwa Watumishi kukuza Ufanisi wa Serikali ya Awamu ya Sita
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi Ajira na Mahusiano Mhe.Deus Sangu amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kwa watumishi wa Ofisi hiyo ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
Mhe. Sangu amesema hayo wakati ya mapokezi ya Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Dkt. Evaline Munisi leo tarehe 6 Mei, 2026, Jijini Dodoma na kueleza kuwa Serikali ya awamu ya Sita imeweka mkazo kwenye uwajibikaji na kutoa huduma bora hivyo amewataka watumishi wote wafanye kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kufikia malengo ya ofisi hiyo.
Aidha, Waziri Sangu amewataka viongozi na watumishi wa ofisi hiyo kushirikiana kwa karibu na Naibu Waziri, Evaline Munisi.
Vilevile, amewahakikishia watumishi kuwa wataendelea kuimarisha mazingira ya kazi, ajira na Mahusiano ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wananchi zinakwenda sambamba na malengo ya Serikali katika kuleta maendeleo nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Evaline Wilbard Munisi amewapongeza na kuwashukuru watumishi wa Ofisi hiyo kwa mapokezi mazuri na kuwaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ili kufanikisha malengo ya ofisi hiyo.
MWISHO
