News
Waziri Sangu awataka waajiri kujisajili WCF na kuwasilisha michango kwa wakati
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, Leo 24 Septemba, 2026 ametembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.
Katika ziara hiyo, Mhe. Sangu amepongeza juhudi zinazofanywa na WCF katika kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma na mafao yanayotolewa na Mfuko, hususan kwa wafanyakazi wanaofanya kazi katika sekta ya madini ambayo ina mazingira yenye vihatarishi mbalimbali vya kiusalama na kiafya.
Amesema WCF ina nafasi muhimu katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata stahiki zao pale wanapopata madhara yatokanayo na ajali au magonjwa yanayohusiana na kazi, na kusisitiza umuhimu wa waajiri kutekeleza wajibu wao wa kisheria kwa kuhakikisha wanawasilisha michango ya Mfuko kwa wakati.
Aidha, Mhe. Sangu amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanajisajili WCF na kuwasilisha michango kwa wakati, ili kuwawezesha wafanyakazi kupata huduma na mafao stahiki endapo watapata ajali au madhara yanayohusiana na kazi, ikiwemo huduma za matibabu, mafao ya ulemavu na fidia kwa wategemezi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha wafanyakazi wanalindwa na kufanya kazi katika mazingira salama na yenye staha.
Mhe. Sangu amesema WCF imeendelea kuboresha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma, ambapo waajiri wanaweza kijisajili na kufanya malipo kwa njia za kidijitali, huku baadhi ya huduma za Mfuko zikipatikana kupitia simu za mkononi, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa waajiri na wafanyakazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, ameeleza ya kuwa WCF inatoa fidia pale mfanyakazi anapopata ajali au ugonjwa unaotokana na kazi na pale ambapo ikitokea bahati mbaya amefariki basi wategemezi wake ikiwa ni mwenza na watoto wake watafidiwa.
