News
Waziri Sangu aziagiza PSSSF, NSSF, WCF na OSHA kuongeza matumizi ya TEHAMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu (Mb) leo (Jumamosi Agosti 8, 2026) amefanya vikao kazi jijini Dar es salaam na Menejimenti za taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji.
Katika vikao kazi hivyo, Waziri Sangu, kwa nyakati tofauti amekutana na Menejimenti za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF); Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF); Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF); na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA).
Waziri Sangu amepokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo kutoka kwa watendaji wake wakuu na kuelekeza taasisi hizo kuendelea kuongeza ufanisi hususan katika matumizi ya teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA) katika utendaji na utoaji huduma kwa wananchi.
“Nawaelekeza kuongeza utoaji wa elimu ya matumizi ya kidijitali katika mifumo yetu ili kuwawezesha wale wasio na elimu ya kidijitali kupata huduma zetu kwa urahisi na haraka,” amesema Waziri Sangu.
Vikao hivyo vilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Hifadhi ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Festo Fute, Wakurugenzi Wakuu wa PSSSF, NSSF, WCF na OSHA pamoja na wajumbe wa Menejimenti za taasisi hizo.
Mhe. Sangu ameendesha vikao kazi hivyo baada ya jana kukamilisha ziara yake ya siku saba katika wilaya zote za mkoa wa Lindi iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali mkoani humo.


