News
Waziri Sangu: Maamuzi bora yanategemea ufuatiliaji na tathmini
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amesema kuwa Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini vinajukumu la kusaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi, kurekebisha pale panapohitajika na kuhakikisha rasilimali za umma zinageuka kuwa na matokeo chanya.
“Wataalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini nyie ndiyo macho, pua na masikio mnaojenga mfumo wa Serikali wa kujua kama mipango tunayoiweka kwenye karatasi inabadilika kuwa matokeo halisi na kuleta tabasamu kwa wananchi,”
Mhe. Sangu amesema hayo tarehe 21 Septemba, 2026 wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Wakurugenzi na Wasimamizi wa Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini Serikalini uliofanyika katika hoteli ya Ngurdoto Mountain iliyopo Jijini Arusha.
Amesema, kutambuliwa kwa jukumu la Ufuatiliaji na Tathmini na kuwa na vitengo vinavyoonekana ndani ya taasisi zetu ni dalili njema ya kwamba Serikali imetambua kuwa haiwezi kupanga vizuri bila kujua
inachofanya; haiwezi kutumia rasilimali vizuri bila kupima matokeo; haiwezi kufikia malengo ya Taifa bila kufuatilia utekelezaji; na haiwezi kujifunza kutokana na uzoefu bila kufanya tathmini.
Aidha, amesema Serikali imewezesha uwepo wa vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala, Mashirika ya umma, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, hivyo zinapaswa kuthamini heshima na uwezeshaji aliofanywa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kutumia kikamilifu nafasi hiyo ambayo imechagiza pia kuwepo kwa mfumo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini Serikalini (Government Wide M&E System), pamoja na mifumo mingine ya kidijitali kama e-Delivery.
Kadhalika, Waziri Sangu ametoa wito kwa Wakurugenzi na Wasimamizi wa Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini kushirikianq, kuwa waadilifu, wazalendo, wabunifu na ujasiri wa kusema ukweli wa data kwa ushahidi halisi.
“Tunapoelekea kwenye utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, tunapaswa kuwa na Ufuatiliaji na Tathmini wa kimkakati unaolenga matokeo na kutoa tahadhari mapema ili kuwezesha ufanyaji wa maamuzi stahiki na kwa wakati stahiki,” amesema
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. James Kilabuko amesema kuwa mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa mwongozo jumuishi wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathmini ambao unatambua umuhimu wa kuwakutanisha Wakurugenzi na Wasimamizi wa Vitengo hivyo ili kubadilishana uzoefu, kutathmini hali ya utekelezaji kwa kukaa pamoja.
Amesema lengo kuu la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwa pamoja wataalamu hao kwa pamoja wanafikia adhma ya kuwa na Taifa lenye uwezo wa kujifunza kutokana na matokeo ya shughuli za ufuatiliaji na tathmini.
Mkutano huo unamefanyika sambamba na maandalizi ya Kongamano la Tano la Kitaifa la Ufuatiliaji na Tathmini (Monitoring, Evaluation and Learning Week) litakalofanyika kuanzia tare 22 Hadi 26 Septemba, 2026.



