News
Afrika na Ghuba zaimarisha ushirikiano kulinda haki za wafanyakazi
TANZANIA imesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za vitendo katika kuhakikisha uhamaji wa nguvu kazi kati ya Afrika na nchi za Ghuba (GCC+) unakuwa salama, wa haki na wenye tija kwa pande zote.
Akizungumza leo (05 Oktoba 2026) jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Pili wa Doha Dialogue, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Zuhura Yunus, alisema mafanikio ya mkutano huo hayapaswi kupimwa kwa ahadi pekee, bali kwa utekelezaji wa hatua madhubuti za kulinda wafanyakazi wahamiaji.
Zuhura, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, alisema ni muhimu kuimarisha mifumo ya uajiri, usalama na afya mahali pa kazi, upatikanaji wa haki, kinga ya jamii pamoja na takwimu za uhamaji wa nguvu kazi.
"Idadi kubwa ya vijana wa Afrika wanaendelea kutafuta fursa za ajira katika nchi za Ghuba, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa usalama na kulinda haki zao," alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Umoja wa Afrika pamoja na nchi za Ghuba ikiwemo Jordan na Lebanon katika kujenga mfumo imara wa ushirikiano utakaohakikisha uhamaji wenye staha wa nguvu kazi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi ya Qatar, Sheikha Najwa bint Abdulrahman Al Thani, alisema nchi za Ghuba zimepiga hatua katika mafunzo ya ufundi stadi, na ziko tayari kushirikiana na Afrika kuwaandaa vijana wenye ujuzi unaohitajika sokoni.
Naye Mkuu wa Idara ya Kazi, Ajira na Uhamaji wa Nguvu Kazi katika Tume ya Umoja wa Afrika, Dk. Sabelo Mbokazi, alisema ongezeko la vijana wa Afrika, hususan kutoka Afrika Mashariki, Magharibi na Kaskazini wanaokwenda Ghuba, linadhihirisha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi hao.
Mkutano huo wa pili umeratibiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Qatar, Tume ya Umoja wa Afrika na nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC), ukiongozwa na kaulimbiu: "Kuendeleza Uhamaji wa Nguvu Kazi wenye Haki na Endelevu kati ya Nchi za Afrika na Ghuba (GCC+)."

.jpeg)


.jpeg)


