Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

Ushirikiano na Utatu wapewa Kipaumbele Mkutano Mkuu wa ILO Geneva


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) unaoendelea jijini Geneva, Uswisi.

Akizungumza Juni 4, 2026, Mhe. Sangu amesema mkutano huo una manufaa makubwa kwa Tanzania kutokana na nafasi yake katika kujadili masuala muhimu yanayohusu haki za wafanyakazi, usimamizi wa viwango vya kazi, na uimarishaji wa stahiki za wafanyakazi kwa mujibu wa mikataba na makubaliano ya Shirika la Kazi Duniani.

Ameeleza kuwa maeneo makuu ya mjadala katika mkutano huo wa mwaka 2026 ni pamoja na maendeleo ya sekta ya kazi duniani, utekelezaji wa mikataba mbalimbali ambayo Tanzania imeridhia chini ya ILO, pamoja na matumizi ya Akili Unde (AI) katika kuimarisha na kulinda kazi zenye staha kwa wafanyakazi.

Mhe. Sangu pia amesema ujumbe wa Tanzania umepata fursa ya kufanya majadiliano na wadau wa utatu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wakiwemo Serikali, Waajiri na Wafanyakazi, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na majadiliano ya kijamii yanayochochea maendeleo ya sekta ya kazi katika kipindi hiki cha ukuaji wa teknolojia na uchumi wa kidijitali.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha ushiriki wa wadau wa utatu katika mkutano huo, hatua ambayo imewapa fursa ya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kuendeleza ustawi wa sekta ya kazi nchini.

Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) umeanza rasmi Juni 1, 2026 na unatarajiwa kuhitimishwa Juni 12, 2026. Mkutano huo unawakutanisha wawakilishi wa Serikali, Waajiri na Wafanyakazi kutoka nchi wanachama 187 wa ILO.