News
Bil.3.8 Kujenga Jengo la Utawala Lindi Manispaa
Serikali ya Awamu ya Sita imetoa kiasi cha Shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kisasa la utawala katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, lengo likiwa ni kuwapatia watumishi mazingira bora ya kuwahudumia wananchi.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha utoaji wa huduma unakuwa bora na unaendana na utawala bora unaolenga kumwezesha mwananchi kupata huduma kwa wakati na staha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, alitoa kauli hiyo Agosti 6, 2026, alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo hilo linaloendelea katika Kata ya Rasbula, Manispaa ya Lindi.
"Wataalamu wa ujenzi hakikisheni bajeti hii ya bilioni 3.8 inakamilisha jengo hili kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa bila kuomba nyongeza nyingine za fedha," aliagiza Waziri Sangu.
Akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo, Waziri Sangu alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekipa kipaumbele kikubwa kuboresha mazingira ya kazi ili wananchi wahudumiwe ipasavyo.
"Rais Samia anataka aache urithi wa tabasamu kwa Watanzania kupitia huduma bora. Ndio maana anahakikisha miradi kama hii inakamilika katika halmashauri zote za Lindi," alisema.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuena Omary, alisema Serikali inakamilisha ujenzi wa majengo ya utawala katika halmashauri zote sita za mkoa huo na kwamba fedha za utekelezaji zinaendelea kutolewa hatua kwa hatua.
Bi. Zuena aliwataka watumishi wa umma mkoani Lindi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ubunifu, kwani Serikali imetimiza wajibu wake wa kuboresha miundombinu ya kazi.
"Tunayo sababu ya kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa Serikali inatuboreshea mazingira," alisisitiza.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mhandisi wa Mkoa wa Lindi, Mhandisi Godfrey Mlowe, alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza mwezi Agosti 2025 na unatarajiwa kukamilika Julai 2027 kwa gharama ya bilioni 3.8 zilizotolewa na Serikali.
Naye Diwani wa Kata ya Rasbula, Mhe. Abdalla Kikwei, alishukuru Serikali kwa kuchagua kata yake kutekeleza mradi huo mkubwa na kuwapongeza wataalamu kwa usimamizi mzuri wa kazi hiyo.
Awali, Waziri Sangu akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Victoria Mwanziva, alitembelea Kituo cha Kulea Wazee wenye Uhitaji mjini Lindi ambapo alisalimiana nao na kukabidhi msaada wake. Waziri aliahidi kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushirikiana na kituo hicho kuhakikisha wazee wanapata huduma stahiki.

.jpeg)

.jpeg)
