News
Bima ya Afya za wezeshwa kwa Wanagenzi
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kuboresha mazingira ya mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi kwa kuwapatia wanagenzi 5,746 bima ya afya na posho ya usafiri ya shilingi 100,000 kwa mwezi kwa kipindi cha mafunzo ya vitendo sehemu za kazi. Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanagenzi kuendelea na mafunzo katika mazingira salama na kuongeza ufanisi wa programu ya taifa ya kukuza ujuzi.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Wilbard Munisi, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi katika Chuo cha Ufundi Stadi St. Anthony, Musoma mkoani Mara, Juni 30, 2026.
Alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya vijana ili kujenga nguvukazi yenye ujuzi, maarifa na ushindani unaohitajika katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Dkt. Munisi alisema maboresho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, inayolenga kuongeza idadi ya Watanzania wenye ujuzi stahiki wa kujiajiri na kuajiriwa huku ikipunguza pengo la ujuzi katika soko la ajira.
Aidha, Naibu Waziri alisisitiza kuwa Serikali inatarajia kuona wahitimu wanaotumia ujuzi walioupata kuibua suluhisho bunifu kwa changamoto za uzalishaji na utoaji huduma nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bi. Alana Nchimbi, alisema kuwa mfumo wa uanagenzi umeendelea kuwa njia bora ya kuziba pengo la ujuzi kwa kuunganisha mafunzo ya darasani na uzoefu wa moja kwa moja mahali pa kazi.
Naye Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi St. Anthony alisema chuo hicho kimepokea wanagenzi 186 wanaofadhiliwa kikamilifu na Serikali katika awamu ya nane ya programu hiyo, huku chuo kikiongeza nafasi kwa wanagenzi wengine 25 kwa ufadhili wa Kanisa Katoliki kutokana na mahitaji makubwa ya vijana waliotuma maombi. Alibainisha kuwa mafunzo yanatolewa katika fani sita zenye mahitaji makubwa katika soko la ajira.
Kwa niaba ya wanagenzi, Neema Abeli aliishukuru Serikali kwa kugharamia ada za mafunzo kwa asilimia 100, kutoa bima ya afya na kuweka utaratibu wa posho ya usafiri kwa kipindi cha mafunzo ya vitendo. Alisema hatua hizo zimeondoa changamoto za kifedha na kuwapa vijana nafasi ya kuzingatia masomo na kujenga ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu, huku akiomba Serikali iendelee kupanua programu hiyo ili vijana wengi zaidi wanufaike.
Mwisho.
