News
Elimu Kuhusu Kutokomeza Utumikishaji wa Watoto yatolewa katika Maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Njombe
Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kutoa elimu katika Maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mjimwema, mkoani Njombe.
Kupitia maonesho hayo, wananchi wamepata fursa ya kuelimishwa kuhusu kazi hatarishi wanazofanyishwa watoto, ambazo huwanyima haki zao za msingi zikiwemo haki ya kupata elimu, huduma za afya, ulinzi dhidi ya unyanyasaji, pamoja na kushiriki michezo na shughuli nyingine muhimu za ukuaji wao.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Elimu Kazi Mkuu, Emiliana Rweyendela, amesema kuwa kwa mujibu wa sheria za kazi nchini, ajira kwa mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 ni kosa. Ameeleza kuwa utoaji wa elimu hiyo unalenga kuongeza uelewa kwa jamii ili kulinda haki za watoto na kutokomeza kabisa vitendo vya utumikishwaji wa watoto.
Kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu ni: “Mazingira ya Kazi Kisaikolojia ni Njia ya Kuimarisha Ustawi wa Wafanyakazi na Kujenga Taasisi Imara.”

