Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

​Kamati ya Bunge Ustawi wa Jamii Yaipongeza Serikali Kutangaza Kima cha Chini cha Mishahara Sekta Binafsi


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imetoa pongezi kwa serikali kwa kutangaza amri ya kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi nchini ambayo inaonyesha dhamira ya kuboresha ustawi wa jamii.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Hawa Mchafu, wakati wa kikao cha Kamati kilichofanyika Bungeni Dodoma leo, Januari 15, 2026, kwa lengo la kupokea taarifa ya muundo na majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano.

“Kwa taarifa ya utekelezaji ya kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, Wizara yenu imefanikiwa vema katika mambo matano ambapo yameonesha namna mlivyoweza kuongeza tija na ufanisi kwenye sekta ya kazi, ajira na mahusiano hatua inayoonyesha ukuaji wa ustawi wa jamii” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Kamati hiyo ya Bunge imesema itakuwa mabalozi wazuri wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha ustawi wa jamii unapatikana, kwa kusisitiza kuwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara zinatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wa Tanzania.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mchafu ameelekeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kuweka mkakati mahsusi wa kushughulikia changamoto tatu kuu, ambazo ni kuendelea kuwepo kwa tatizo la ajira kwa watoto, baadhi ya waajiri wa sekta binafsi kushindwa kuwasilisha michango katika mifuko ya hifadhi ya jamii, pamoja na kufanya ufuatiliaji wa tatizo la mikataba ya ajira za muda mfupi kwa Watanzania kukatishwa bila kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Akiwasilisha taarifa kuhusu muundo na majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo Mheshimiwa Deus Sangu, aliwaeleza Waheshimiwa Wabunge kuwa Ofisi imelenga kikamilifu kutekeleza majukumu ili kukuza ustawi wa jamii ya watanzania katika sekta za Kazi, Ajira na Mahusiano.

Waziri Sangu alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2025 ikiwemo kutangazwa kwa kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi Namba 606A ambayo imeanza kutumika rasmi mwezi Januari 2026 na kuanzishwa kwa mafao ya pensheni na akiba kwa wanachama wa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi waliojiajili.

Mafanikio mengine ya Ofisi aliyoyataja ni kukamilika kwa maandalizi ya uzinduzi na uvumishaji wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 ambayo itazinduliwa mwezi Februari 2026, kuongeza ujuzi kwa wakulima na waasindikaji wadogo 1,000 katika mikoa minne ya Dodoma, Singida, Iringa na Mbeya, pia kuratibu upatikanaji wa ajira nje ya nchi ambapo jumla ya watanzania 1,432 wameunganishwa na fursa hizo hadi kufikia Novemba 2025.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa kamati hiyo wameshauri mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza katika miradi ya maendeleo ya kimakakati itakayozalisha ajira kwa vijana nchini pamoja na kupongeza mifuko kwa kuimarisha matumizi ya TEHAMA ambayo yameboresha utoaji huduma kwa wanufaika.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa muundo na majukumu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Fortunatus Magambo alisema mfuko huo umeendelea kuwa himilivu na kuongeza kasi ya kulipa mafao kwa wanachama wake nchini.

Kikao hicho cha Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imepokea taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ambapo kesho itaendelea na taasisi zingine za wizara ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Watumishi (WCF), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA).