News
Kamishina Mtanda aipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuunganisha Watanzania na Ajira za nje ya Nchi
Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia Divisheni ya Pasipoti na Uraia nchini, Ally Mohamed Mtanda, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kuwaunganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi.
Ametoa pongezi hizo Julai 10, 2026, alipotembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2026.
Kamishna Mtanda amesema juhudi hizo zinaendelea kuleta maendeleo kwa wananchi mmoja mmoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha Kamishna Mtanda alipendekeza Kitengo cha Huduma za Ajira kuendelea kushirikiana kwa karibu na Idara ya Uhamiaji kutoa mafunzo kwa wananchi wanaopata fursa za Ajira nje ya nchi kabla ya kuondoka, amesema mafunzo hayo yatawajengea uelewa kuhusu haki zao za msingi, na masuala ya usalama wanapokuwa nje ya mipaka ya Tanzania.
Vile vile, ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kushirikiana na balozi za Tanzania zilizopo nje ya nchi ili kubaini na kutangaza fursa mbalimbali za ajira zinazopatikana, hatua itakayowawezesha Watanzania wengi zaidi kunufaika na soko la ajira la kimataifa.

.jpeg)
